Chini ya kisingizio cha kupambana na COVID-19 kunafanywa bidaa mpya kwa Dini yetu

Taarifa kwa Vyombo Vya Habari

Serikali kupitia baraza la dini mseto (Inter- Faith) imefungua misikiti kwa mikakati mikali. Jopo hilo la wanachama kumi na tano lilipewa jukumu la kufanyakazi na wizara ya mambo ya ndani pamoja na wizara ya afya katika kuweka masharti ya kufunguliwa tena maabadi.Kati ya masharti hayo yanayopaswa kufuatwa kwenye nyumba za ibada ni; kuweka umbali wa masafa ya mita 1.5 baina wanaoswali, idadi ya watu 100 pekee kuruhusiwa kuabudu, watoto chini ya umri wa miaka 13 na watu wazima wenye umri wa miaka 58 kutoruhusiwa kuingia kufanya ibada na muda wa kufanya ibada usizidi saa moja.

Kwa haya, tungependa kueleza yafuatayo:

Fikra jumla ya maingiliano ya kiimani ni fikra ya kisekular isio na msingi wowote katika Uislamu.Hii ni kuwa fikra hii inatoa mwito wa kuweko na uiano baina ya imani mbalimbali za Kidini.Fikra hii aidha inalingia dini nyengine mpya kinyume na Uislamu ambayo Wamagharibi wanataka Waislamu wote kote duniani kuikubali dini hiyo. Binafsi wazo hili linalenga kuwafanya Waislamu waachane na mafundisho yao Kiislamu badali yake fikra za kisekular iwe ni kipimo cha Dini yao.

Sheria za Kiislamu zimetoka kwa MwenyeziMungu SWT (Wahyi),katu hazibadilishwa na mamlaka yoyote yale, tofauti na  kanuni za Kisekular zinazotokamana akili za mwanadamu hivyo huwekwa na kubadilishwa kulingana na mazingira. Na ndio kwa muktadha huu, twakumbusha masheikh ambao baadhi yao ni wanajopo wa baraza la Interfaith, walichotakikana ilikuwa ni kuweka bayana sheria za Kiislamu kuwa hazichukuliwi mahala popote pale ila kwenye machimbuko yake asili ambayo ni Quran, Sunna na Ijmaa na Qiyas.Hili ndilo jukumu la wanavyuoni wamchao Mungu nao hupaza kauli ya haki pasina kuogopa ya lawama ya mwenye kulaumu.

Utekelezwaji wa ibada ya Swala za Jamaa umeonyeshwa kivitendo na Mtume wetu Muhammad (Saw), hivyo si suala la kufanyiwa mashauriano. Kwa hali hii, ni faradhi kwa Waislamu wote kupanga safu wakiwa kwenye swalah pasina kuacha mwanya baina ya mtu mmoja na mwengine. Amepokea Almaalik Bin Al-huwairith Radhi za MwenyeziMungu zimshukie kwamba Mtume (Saw) alisema:

وَصَلُّوا كَمَا رَأَيْتُمُونِي أُصَلِّي وَإِذَا حَضَرَتِ الصَّلَاةُ فَلْيُؤَذِّنْ لَكُمْ أَحَدُكُمْ ثُمَّ لِيَؤُمَّكُمْ أَكْبَرُكُم

Na swalini kama mlivyoniona nikiswali na inapowadia Swala, basi mmoja wenu aadhini kisha yule mkubwa wenu kiumri aweze kuwaswalisha.

Na akapokea Imam Ahmad kutoka kwa Abdullah Ibn Umar kuwa Mtume (Saw) alisema:

«أَقِيمُوا الصُّفُوفَ فَإِنَّمَا تَصُفُّونَ بِصُفُوفِ الْمَلَائِكَةِ وَحَاذُوا بَيْنَ الْمَنَاكِبِ وَسُدُّوا الْخَلَلَ وَلِينُوا فِي أَيْدِي إِخْوَانِكُمْ وَلَا تَذَرُوا فُرُجَاتٍ لِلشَّيْطَانِ وَمَنْ وَصَلَ صَفّاً وَصَلَهُ اللَّهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى وَمَنْ قَطَعَ صَفّاً قَطَعَهُ اللَّهُ»

Simamisheni safu  kwani  safu zenu zinakua pamoja na za Malaika safu na muoanishe bega kwa bega, zibeni mianya na wafanyieni upole ndugu zenu na wala msiache mianya ya shetani. Atakayeunga safu MwenyeziMungu Naye atamuunga na mwenye kukata safu MwenyeziMungu naye atamkata.

Ni bayana kutokana na dalili hizo hapo juu kwamba kuwalazimisha wenye kuswali kuweka umbali wa mita1.5, sawa iwe ni swala za Jumua ama za Jamaa kwa hofo ya maambukizi hasa ikiwa wale waumini hawana dalili kabisa za maambukizi kitendo hiki ni uzushi katika Uislamu. Fauka ya haya, maradhi ya maambukizi ni udhuru wa kisheria wa waislamu kutokwenda msikitini wala sio udhuru wa kuruhusu kuenda msikitini kisha kujiweka mita moja toka kwa mwengine wakati wa kuswali.

Kuhusiana na sharti ya kuruhusu watu 100 pekee kuingia msikitini, kuwazuia watu wazima wenye umri wa 58 na watoto chini ya umri wa miaka kumi na tatu,kitendo hiki sio kuwa hakigongani tu na mafundisho ya Kiislamu bali pia dhulma dhidi ya waumini Wakiislamu na ni jambo lisilomridhisha MwenyeziMungu SWT. Na mgongano mkubwa wa maadili ya uongozi kwa kuweka masharti magumu kwa wanaoswali ilhali barabarani, ofisini, maduka na maeneo mengine bado tunayaona yakifurika watu pasina masharti hayo ya umri.Je hii ina maanisha kwamba maradhi ya Covid-19 huweza tu kuambukizwa ndani ya Misikiti wala sio kwengineko na kwa hivyo ni lazima ifunguliwe kwa idadi maalumu ya waumini wenye umri maalum?!

Tunasisitiza kuwa janga hili ni changamoto na mtihani kutoka Muumba Aliyetukuka kwa waja wake ukitutaka kurudi Kwake Yeye kwa kwa kutubia na kunyenyekea kwa maamrisho yake. Kwa munasaba huu, kufunguliwa kwa misikiti kwa masharti magumu ambayo yanagongana na sheria za MwenyeziMungu kunafanya vifua vya vya Waislamu kuungulika kwa maumivu makali. Hata hivyo, tunafahamu kwa yakini kuwa kwa kusimamisha tena Khilafah  kupitia njia ya Utume katika moja ya mataifa makubwa ya Kiislamu, Misikiti hivi karibuni itatukuzwa na Jina la MwenyeziMungu kutajwa ndani yake asubuhi na jioni.

 

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo Vya Habari

Hizb ut Tahrir in Kenya

KUMB : 1441 / 12AH

Thursday, 26th Dhul-Qaada 1441 AH/

16/07/2020 CE