Idd ul-Fitr Inatujia Ilhali Uislamu, Waislamu na Wanadamu Jumla Wamo Katika Kiza!

Ijumaa hii ni ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani Mwaka huu wa 1440H. Mwezi huu huingia ukiwa umejaa baraka tele kwa Waislamu kwani pia hukumbuka kushukishwa kwa Qur’an tukufu muongozo wa wanadamu wote. Kumalizika kwa mwezi huu kunatakiwa kuache athari ya kudumu ya kuenzi utukufu wa Qur’an na kuitendea kazi maishani mwetu. Asema Mwenyezi Mungu (swt):

(شَہۡرُ رَمَضَانَ ٱلَّذِىٓ أُنزِلَ فِيهِ ٱلۡقُرۡءَانُ هُدً۬ى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَـٰتٍ۬ مِّنَ ٱلۡهُدَىٰ وَٱلۡفُرۡقَانِ‌ۚ)

“Ramadhani ni mwezi ambao Qur’an imeteremshwa kuwa ni uongofu (muongozo) kwa watu, hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi”

[Al-Baqarah: 185]

Lakusikitisha ni kuwa Ramadhani huingia na kutoka ilhali hali ya Uislamu na Waislamu bali Wanadamu jumla inaendelea kuwa mbaya kila kukicha. Hii ikitokamana na kutawaliwa na mfumo batili wa kirasilimali ambao itikadi yake ni usekula/uilmaniyya (kutenganisha dini na maisha/serikali). Hivyo basi kuipa daraja akili ya mwanadamu iliyo na kikomo kuwa ndiyo iliyo na upeo wa juu wa kutunga sheria na kujiongoza maishani/serikalini. Natija yake ni kuchipuza kwa nidhamu ovu zinazotokana na mfumo huo. Miongoni mwa nidhamu hizo ni nidhamu ya kiutawala ya kidemokrasia ambayo imempa ubwana mwanadamu kuendesha mambo anavyotaka, nidhamu ya kijamii iliyosimama juu ya msingi wa uhuru kiasi kwamba kuwapelekea wanadamu kuwa duni kuliko hata wanyama, nidhamu ya kiuchumi iliyo makinishwa juu ya msingi wa uporaji mali za watu kwa njia za utozaji ushuru na mikopo ya riba, nidhamu ya kielimu inayolenga kujenga utambulisho wa kisekula (Shaksiyyatul Ilmaniyya) na nidhamu ya mahusiano ya kigeni iliyokitwa katika msingi wa ukoloni n.k!

Hakika hali duni na ya kukatisha tamaa inaendelea kushuhudiwa ulimwenguni kote ikiwemo mpaka ndani ya Dola zinazodaiwa za ulimwengu wa kwanza ikiwemo Marekani, Uingereza, Ufaransa n.k. Yote ikiwa chimbuko lake ni kufuata muongozo batili wa mfumo wa kirasilimali! Wakati umefika kwa wanadamu kuutizama Uislamu kama mfumo badala uliowahi kwa karne 13 kusuluhisha matatizo yaliyoukumba ulimwengu. Kwani Uislamu ni muongozo sahihi unaotoka kwa Mwenyezi Mungu (swt), Muumba wa ulimwengu, mwanadamu na uhai. Kwa kuwa tunakwenda kinyume na muongozo wake basi Naye (swt) ametuambia:

(وَمَنۡ أَعۡرَضَ عَن ذِڪۡرِى فَإِنَّ لَهُ ۥ مَعِيشَةً۬ ضَنكً۬)

“Na atakeye jiepusha na mawaidha (muongozo) yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki” [TaHa: 124]

Hivyo basi, wanadamu jumla hawana budi isipokuwa kurudi kwa muongozo wa Muumba wao na sio mwengine isipokuwa ni Uislamu kama mfumo mkombozi kwa wanadamu. Fauka ya hayo Waislamu hii ndiyo nafasi ya kupatiliza kurudi kwa Mwenyezi Mungu (swt) kwa kurudisha maisha ya Kiislamu kwa kusimamisha Serikali ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume. Ni kupitia Khilafah kwa njia ya Utume ndiko kutakakopelekea ukombozi wa Uislamu, Waislamu na Wanadamu jumla kutoka katiza cha kutawaliwa na ukafiri ambao umesababisha majanga katika nyanja za maisha! Na kuleta utulivu na ufanisi wa kweli.

Tukiwa tupo katika pingu za mfumo batili wa kirasilimali na itikadi yake ya kipagani ya kisekula, siku kuu ya Iddul-Fitr bado haijakuwa ni siku ya furaha kwa Waislamu wote kwa ujmla. Waislamu wengi katika mataifa mengi ya Waislamu watakuwa wanakaribisha Idd kwa hofu ya mashambulizi kutoka kwa watawala wao vibaraka!  Mara nyingi Idd zetu hutujia ikiandamana na ufuska wa hali ya juu unaotokamana na fikra huria zinazowafanya wanadamu kutokuwa na heshima wala utu!  Suluhisho la matatizo tunayokumbana nayo ni kuung’oa mfumo huu pamoja na wapigiaji debe wake wakijumuisha watawala vibaraka katika ardhi za Waislamu waliowekwa mamlakani na Wakoloni Wamagharibi. Hili likiwezekana kupitia ndugu zetu mukhlisina wanajeshi waliomo ndani ya kambi za kijeshi kutoa nussrah na kusimamisha Khilafah ili tutawaliwe kwa Shari’ah (Qur’an na Sunnah) chini ya Mtawala Mmoja, Khalifah ndani ya Dola Moja kama Ummah Mmoja.

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Makala Na.47: Ijumaa, 26 Ramadhani 1440 | 2019/05/31