Janga la Corona lazidisha Janga jengine la uvundo wa ubaguzi

Katika hatua za serikali ya Uchina za kupampana na jinamizi la virusi vya Corona, waafrika waishio nchini humo wanalilia usaidizi wa dharura kutokana na kufanyiwa vitendo vya kinyama. Ripoti zinazoambatana na picha za video zinaonyesha hali ya kutamausha ya raia wakiwa wanalala barazani wakipigwa na baridi kali na hii baada ya kufurushwa na wenye nyumba. Visa vya kubaguliwa wanapoingia kwenye maduka makubwa na wengine wakishambuliwa kwenye vyombo vya usafiri pia vimeripotiwa. Kwa mujibu wa raia wa Kenya waishio maeneo ya Guangzhou na Guangdong, ni kuwa wenyeji wao wamekuwa wakifanyiwa unyanyapaa kwa madai ya kuwa wanasambaza maradhi ya Corona.

Huku raia barani Afrika wakiwa wameghadhibishwa na ukatili huo dhidi ya waafrika wenzao huko China, serikali za Kiafrika kwa upande wake zimepatwa na kigugumizi baina ya  kukashifu kimdomo unyama huo ama kubakia tu kuulaumu uongozi wa Chini kwa madhila dhidi ya  raia wao. Kwa mfano, huku Kenya ikisema kwamba imelalamikia China kwa ukatili unaofanywa dhidi ya wakenya kwa upande mwengine, inaonekana ikitetea hatua za Beijing kuwa imechukua hatua mpya za Uchina za  kuwapima watu ili kudhibiti maambukizi ya Covid-19. Tarehe 10, Aprili, waziri wa mambo ya nje wa Kenya Raychelle Omamo alisema serikali ya Kenya imetuma malalamishi yake kwa Uchina juu ya masaibu hayo. Ubalozi wa China Jijini Nairobi kwenye mazungumzo yake na gazeti la The Star, unadai kwamba video zinaoneshwa hazina uhalisia wa maelezo kamili na kwamba waafrika wengi huko china walikiuka mikakati ya kiafya kama kuepuka maeneo yenye mikusanyiko ya watu na kuvaa vibarakoa/vitanzua. Na baadae ikadaiwa kuwa wakaonyesha dalili za maambukizi na huku washaambukiza watu”

Kwa mwenye kuiangalia historia, ataona wazi jinsi utawala wa Kichina ulivyosheheni rekodi mbovu ya matumizi ya hatua za kikatili sio tu kwa raia wa Kigeni bali hata raia wake wanaonekanwa kupinga matendo yake maovu. Kabila la kichina la Han – ambalo ni kubwa zaidi duniani linalochangia asilimia 18 ya idadi ya watu duniani limekua likatambulika kwa vitendo vyake vya ubaguzi. Mwanahistoria Yan Shigu akitoa maoni yake kwenye kitabu kiitwacho Book of Han anaelezea jinsi  jamii hii  ilivyokuwa ikitusi jamii ya Wusun na kuibeza  kwa kuitwa jamii ya kishenzi walio na macho ya kijani na nywele nyekundu’ kulingana na Abu Zayd Hasan wa Siraf ni kwamba kundi mmoja la kiusai lilihusika katika mauaji ya halaiki ya Guanzhou (Guanzhou massacre) ambapo  wafanyibiashara wa kiarabu, mayahudi na wakristo waliuwawa.Kwa sasa hivi, ulimwengu unafahamu wazi jinsi Waislamu wa jamii ya Uighuri wanavyowekwa kwenye makambi hatarishi, kuzuiliwa kwao kuswali na kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Uovu huu  unaonyesha wazi namna ya sera za kiubaguzi leo zilivyozagaa sio tu kwa ngazi za raia wa kawaida bali hadi katika safu za watawala. Wanasiasa wa kimagharibi na kimashariki wamekuwa mara kwa mara wakitoa semi za chuki na ubaguzi dhidi ya watu weusi. Ni hivi karibuni tu rais wa Amerika, Donald Trump alikejeli mataifa ya kiafrika ‘mataifa ya shimo la choo’.Kinaya ni kwamba,Marekani kwa sasa anaikashifu China kwa kubagua watu weusi katika janga hili la Corona.  Kulingana utafiti wa kituo cha utafiti cha Marekani cha  Pew ni kwamba nchini Marekani kila kwenye watu weusi elfu moja,kuna  mtu mmoja huawawa na polisi. Wamarekani  weusi hufariki dunia zaidi kutoka na kupigwa na polisi kuliko wamarekani weupe kwa kiwango cha asilimia zaidi ya 2.5. Ama katika mataifa ya Afrika, nako pia upandikizaji wa chuki za kikabila na kieneo ni wenye kushuhudiwa. Mambo haya maovu ndiyo kihakika  zana ya kisiasa kubwa ya wanasiasa wengi barani  wanayoitumia  kufikia ajenda zao za kisiasa. Miaka ya hivi karibuni taifa ambalo lilidai kujengwa juu ya misingi ya kuunganisha Waafrika pamoja –Afrika Kusini,wazururaji wamekuwa wakisababisha ghasia katika jiji la kibiashara la Johannesburg, huku wakichoma moto majumba na kupora mali za waafrika wa mataifa mengine wanaopachikwa jina la wahamiaji! Mwaka jana, mbunge wa eneo la Starehe Jijini Nairobi Charles Njagua Kanyi ‘Jaguar’ alishtakiwa kwa mashtaka ya kutumia semi za uchochezi dhidi ya raia wa mataifa ya Tanzania, Uganda, Pakistan na China kwa kile alichokitaja kama wamechukua nafasi za raia wa Kenya kibiashara Jijini. Tukio hili lilikuja siku kadhaa baada ya  serikali ya Kenya kuwarudisha makwao  raia saba wa Kichina kwa hoja ya kuuza nguo za mitumba katika soko la Gikomba, Nairobi.

Hulka mbovu ya kuwabagua wanadamu kwa misingi ya rangi, kabila, lugha, na eneo ni yenye kutapakaa kote duniani. Dhambi hili  linapaliliwa zaidi na wanasiasa wanaonufaika na njama ya kikoloni unaojulikana kama Sykes –Picot- (Hatua ya wakoloni kuugawa ulimwengu kimapaka kama njia moja wapo ya kuendeleza ukoloni wao dhidi watu.) Kwa hakika mradi huo ndio unaofanya chuki za kimapaka na uadudi uweze kutawala pembe zote duniani. Visa vya kubagua raia wa mataifa mengine vinaonesha wazi fikra duni za utaifa na uzalendo kamwe hazifai kuwa misingi wa kuwafungamanisha wanadamu.

Uislamu ndio mfumo pekee ulio na njia bora za kufungamanisha wanadamu kwa umoja wa kudumu unaowadhaminia utulivu na amani mahala popote waishipo. Katika historia yote ya mwanadamu ni Uislamu pekee ndio ulioweza kuunganisha watu wa tabaka mbalimbali pasina na kuzingatia rangi, kabila , lugha na eneo na kuwa umma mmoja. Katika kipindi cha utawala wa Serikali ya Kiislamu viongozi wake (makhalifa) waliweza kufungua miji ya Iraq, Sham, mashariki mwa bara Ulaya, na kaskazini mwa Afrika. Maeneo yote hayo yalikuwa na wenyeji wenye dini na mila tofauti. La kuvutia ni kwamba hakuna uongozi wa Kiislamu haikuripotiwa ndani yake visa vya kiubaguzi jambo lililopekekea wakaazi wa miji hiyo kuupenda Uislamu na sheria zake hata kama wengine hawakuamini! Na kabila nyingi katika maeneo mengi yaliingia katika Uislamu na kuwa ndugu wa dhati wa kiimani umma mmoja uliojengwa juu ya itikadi moja ya Laa ilaha ila LLah. Ikawa hakuna tofauti baina ya mabarbari wa Afrika kaskazini na Masindh wa Pakistan, wasyria na maarmenia, waroma na waarabu wote wakawa ndugu wakipendana na kufahamu kwamba hakuna ubora kati yao ila kwa uchaji mungu.

Basi kama ulivyofaulu Uislamu kuondosha fikra za kikabila, ubaguzi na uzalendo hivyo hivyo ndivyo unavyotarajiwa inshallah chini ya serikali ya Khilafah kupiga vita fikra zote hizo kwani ni uvundo. Yoyote yule atakayepatikana akilingania fikra hizi atakashifiwa vikali na kupewa onyo kali. Kwa nini isiwe hivyo ilhali Uislamu umetangaza wazi kuwa hakuna tofauti ya baina ya mwarabu na asokuwa mwarabu, mweupe na mweusi ila ubora uko kwa kufuata maamrisho ya MwenyeziMungu SWT. Kwa msingi huu sheria za Kiislamu zitamuandama yoyote yule pasina na kuangalia cheo chake na kabila lake Muislamu ama asiyekuwa Muislamu.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ لِلَّهِ شُهَدَاءَ بِالْقِسْطِ ۖ وَلَا يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَىٰ أَلَّا تَعْدِلُوا ۚ اعْدِلُوا هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ ۖ وَاتَّقُوا اللَّهَ ۚ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ

Enyi Mlioamini: Kuweni Wasimamizi wa (kupitisha haki) kwa ajili ya MwenyeziMungu muwe mkitoa shahada kwa uadilifu. Walakuchukiana na watu kusiwapelekeeni kutowafanyia insaf (uadilifu). Fanyeni uadilifu huko ndio kunakomkurubisha mtu na ucha-Mungu. Na mcheni Mungu hakika ya MwenyeziMungu ni mwenye habari kwa yote myatendayo.

[TMQ: AL-MAIDA:08 ]

 

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari

Hizb ut-Tahrir Kenya.