Mfumo wa Kibepari: Janga Juu ya Majanga

Taarifa kwa Vyombo Vya Habari

Makumi ya maelfu ya watu kote nchini wameathiriwa na mvua kubwa, mafuriko na maporomoko ya ardhi. Kenya, ikiwa ni pamoja na Pembe ya Afrika imekumbwa na mvua kubwa inayohusishwa na hali ya hewa ya El Nino katika wiki za hivi karibuni iliyosababisha vifo vya makumi ya watu, ikiwa ni pamoja na zaidi ya 100 katika maeneo mbalimbali ya Kenya. Uharibifu mkubwa wa nyumba na barabara umetokea.Hizb ut Tahrir / Kenya ingependa kutaja yafuatayo:-

Tunahuzunishwa na vifo vya watu na uharibifu wa mali na kwa haya tunatoa mwito kwa jamii nzima ya Kenya na hasa Waislamu kuweza kutoa misaada kwa wahanga kwani hili ni miongoni mwa mambo yanayohimizwa na Uislamu. Mtume Rehema na Amani za MwenyeziMungu  zimshukie alisema:

«مَنْ فَرَّجَ عَنْ مُسْلِمٍ كُرْبَةً، فَرَّجَ اللَّهُ عَنْهُ كُرْبَةً مِنْ كُرُبَاتِ يَوْمِ القِيَامَةِ» “

(Yoyote atakayemuondoshea Muislamu  dhiki yoyote ile basi MwenyeziMungu atamuondoshea dhiki miongoni mwa dhiki za siku ya Qiyama}

Majanga kama haya yanapotokea, hutulazimisha kutambua  udhaifu wa wanadamu na kuthibitisha uwezo wa MwenyeziMungu swt Muumbaji wa Mwanadamu, Uhai na Ulimwengu. Huu ni ushahidi wenye nguvu wa kuthibitisha kwamba kimaumbile mwanadamu, mwenye mipaka ni yuko chini ya nguvu zilizo nje ya uwezo wake hivyo huhitajika na kuwa na mwongozo wa Muumba wake MwenyeziMungu unaosimamia mambo yake yote maishani utakaomdhaminia ufanisi mkubwa.

Mafuriko hayo yameonyesha wazi kushindwa kwa uhandisi wa miundombinu kutokana na ufisadi wa kisiasa ambao umeathiri kabisa ujenzi huo. Kwa muktadha huu, idadi ya watu kwa ujumla itabeba mzigo maradufu wa ushuru na ujenzi duni kutokana na ufisadi.

Mara nyingi majanga hayo yanapotokea, hudhihirisha hali halisi ya itikadi ya kimatata ya kibepari na mifumo yake ya utawala ya kutopeana kipaumbele kwa maslahi ya umma. Lakini la ajabu kwenye michakato ya  kuwania madaraka, wanasiasa wa kibepari huzunguka nchi nzima kwa helikopta kutafuta kura huku kwenye mafuriko wanakodolea macho televisheni raia wanapo kufa maji!  Hii ndiyo taswira halisi ya ubepari na viongozi wao wanaothamini maslahi yao kibinafsi na  kutojali maisha ya maskini.

Mwisho wa yote ni kwamba serikali ndio inayopaswa kubebeshwa kidole cha lawama kwa kutepetea juu ya usalama wa watu kwani ilipaswa kuchukua hatua za tahadhari kwa kuweka taratibu maalum kama njia ya kupunguza athari hizo za maafa pamoja na hatua za haraka za kuwaokoa watu.

Uislamu kama mfumo kamili wa  kimaisha umeanisha kwamba jukumu la kusimamia mambo ya umma kimsingi ni la serikali na wala sio kwa raia au mashirika ya kibinafsi. Mtume Muhammad Rehema na Amani Zimshukie alisema:

«الإِمَامُ رَاعٍ وَهُوَ مَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ» “

Imamu/ Kiongozi ni mchungaji na ni mwenye kuulizwa juu ya wale anaowachunga.

Kuhusu majanga kama mafuriko, Uislamu umemuamuru kiongozi kutumia fedha kutoka hazina (Baitul Mal) kuwahudumia raia walioathirika  na hili ni jukumu lake juu yao wala sio fadhila kwao. Ikitokea hakuna fedha kwenye hazina ya serikali, basi kiongozi analazimika kuwatoza tajiri kiasi maalum cha kodi ili kufidia hali hiyo. Na hivi ndivyo Khilafah inavyotazamiwa kusimamia maslahi ya raia wake Kwa idhni ya Allah Ta’ala.

Shabani Mwalimu
Mwakilishi Kwa Vyombo Vya Habari Hizb ut Tahrir Kenya