Njia ya Mtume (saw) Kuleta Mageuzi

بسم الله الرحمن الرحيم

Halaqa 9: Kuvumilia Shida na Maudhi kwa Abdullahi Ibnu Masoud na Mus’ab Ibnu Umair Katika Da’wah

Katika halaqa hii tutamalizia mbinu ya nne na ya mwisho ambayo wameitumia Maquresh dhidi ya da’wah ya Mtume (saw). Na leo tutazungumzia maudhi na adhabu ambazo wamezipata baadhi ya Maswahaba Radhi za Allah ziwaendee.

Wa kwanza aliye dhihirisha Uislamu

Ameelezea Zubeyr ibnul Awwam (ra) asema: Wa kwanza aliye dhihirisha Uislamu baada ya Mtume (saw) katika mji wa Makkah ni Abdullah Ibnu Masoud (ra) walipo kusanyika maswahaba wa mtume (saw) wakasema: Maquresh hawajaisikia Qur’an ikisomwa wazi kabisa. Je Nani atawasikilizisha? Akasema Abdullah Ibnu Masoud: Mimi

Wakasema: Sisi tunakuogopea, sisi tunataka mtu ambaye ana jamaa watakao mhami kutokana na hawa watu wakitaka kumfanyia ubaya…. Akasema: Niacheni Allah Atanihami…! Kesho yake Ibnu Masoud alipo pambaukiwa Alikuja katika Maqam wakati wa dhuha/asubuhi na Maqureysh wako katika shughuli zao. Akasimama katika Maqam kisha akasoma kwa sauti juu aya hii:

الرحمن علم القرآن

Mwingi wa Rehma, Amefundisha Qur’an.

[Ar-Rahmaan: 2]

Kisha akawaelekea huku anasoma wakasikiza kwa makini huku wanasema: Anasema nini mtoto wa mama mtumwa…? Hakika anasoma baadhi ya aliyo kuja nayo Muhammad… wakamwenukia wakawa wanampiga usoni mwake, na yeye anaendelea na kisomo chake mpaka akafika katika kisomo kiasi Allah anachotaka afike…

Kisha akarudi kwa maswahaba (ra) wenzake ilhali amepigwa usoni mwake na katika mwili wake, wakamwambia: haya ndio tuliyo kuwa tunayaogopea kwako…! Akasema: Maadui wa Allah hawaja wahipo kuwa madhalili kwangu kuliko sasa, na mkitaka kesho pia nitawaendea…! Wakasema: hapana tosha hiyo kwani umewasikilizisha wanachokichukia…!

Balozi wa kwanza wa Uislamu

Mus’ab Ibnu Umair, ni mmoja wapo miongoni mwa wale waliofundishwa adabu na Uislamu, na akalelewa na Muhammad (saw). Hakika kisa cha maisha yake yana Sharaf kubwa kwa wanadamu…!

Alisikia kuwa Rasul (saw) na walio pamoja naye wanajumuika katika nyumba ya Arqam Ibnu Abiy Al-Arqam, Akaenda huku ana mahaba, na kwa upepesi wa jicho akasilimu na akamficha mamake Uislamu wake…!

Alionekana na Uthman Ibnu Twalha akiingia katika nyumba ya Arqam kwa kujificha kisha akaonekana tena mara ya pili akiswali kama swala ya Muhammad (saw) huyu bwana akaenda upesi kumpa habari mamake. Kwa haraka mama akatangaza kukasirishwa kwake na Mus’ab kwa sababu Ameigura miungu.

Alisimama Mus’ab mbele ya mamake na jamaa zake na mbele ya mabwenyenye wa kiquraysh walio kusanyika mbele yake akawasomea Qur’an kwa yakini na thabat ambayo Muhammad (saw) huosha mioyo yao nayo na kujaza kwayo hikma na nguvu, sharaf na uadilifu na uchamungu…!

Alikuwa Mus’ab kabla ya kusilimu kwake ni kijana anaye julikana mwenye neema aliye zaliwa katika neema na akakulia katika neema, na akawa barobaro katika hali hii. Mamake alipokata tamaa ya kuritadi kwake alimnyima kila kitu alichokuwa akimpa, akakataa asile chakula chake mtu aliye igura miungu, akamlaani, hata kama huyu mtu ni mtoto wake…!

Si haya tu, bali aliendelea mamake na vikwazo akamfungia katika chumba akawa humo mahabusu, mpaka walipotoka baadhi ya Waumini wakigura kwenda Habasha naye akajitolea na kuwahepa walinzi na mamake, akaenda Habasha…!

Mus’ab aliiandaa nafsi yake abadili maisha yake kwa maisha mapya ambayo muongozo wake amepewa na Muhammad (saw). Alitoka siku moja na baadhi ya Waislamu wakiwa wamekaa kando ya Mtume (saw) walipo muona wakainamisha vichwa vyao na kufumba macho yao wengine wakatokwa na machozi mengi sana hilo ni kwa kumuona Mus’ab amevaa joho lenye viraka wakakumbuka hali aliyokuwa nayo mwanzo kabla ya kusilimu, alipokuwa na nguo kama maua na bustani inayopendeza na mafuta mazuri yanayonukia…!

Alipo muona (saw) alisema: “Nilimuona Mus’ab huyu, na Makkah hakukuwa na kijana aliye pata neema/mazuri kwa wazazi wake kama yeye, na amewacha yote hayo kwa mapenzi ya Allah na Mtume wake…!”

Kisha Mtume (saw) akamchagua kwa jukumu muhimu…! Alimchagua awe balozi kwa mji wa Madina, anawafundisha Maanswar ambao walimpa bay’ah katika Aqabah na kuwaingiza wengine katika dini, na kuiandaa Madina kwa siku ya Hijra kubwa.

Alifaulu Mus’ab Ibnu Umair kufaulu kuso na mfano! Alienda Madina siku aliyotumwa na Rasul (saw) na Madina hamna Waislamu isipokuwa 12 tu lakini yeye alikaa nao miezi ya kuhesabika mpaka wakakubali watu wa Madina mwito wa Allah na Mtume wake (saw), hakukubakia nyumba katika mji wa Madina ila kunatajwa Uislamu ndani yake…!

Na katika msimu wa Hijjah uliofuatia bay’ah ya Aqabah Waislamu wa Madina walikuwa wakituma wajumbe wanao wawakilisha… Na ikawa idadi ya Wanachama ni kundi la Waumini sabiini na mwanamke mmoja (71) walihudhuria kutekeleza amali za Hijjah, waliulizana wao kwa wao: “mpaka lini tutamuacha Mtume (saw) anafukuzwa kwenda katika majabali ya Makkah na akiogopa…?

Walipofika Makkah kukapita kati yao na Mtume (saw) mawasiliano ya kisiri yaliyo pelekea baya’h ya Aqabah ya Pili ambayo ilijulikanwa baada ya hapo kuwa ni Bay’atul Harb.Hii ilikuwa kabla ya kusimama serikali ya Kiislamu.

Baada ya kusimama serikali ya Kiislamu chini ya Uongozi wa Mtume (saw), Mus’ab (ra) alibeba bendera siku ya Uhud, Waislamu walipolemewa yeye alibaki uwanjani, Ibnu Qumaiah alimfuata akampiga Mus’ab mkono wa kulia na kuukata, Akashika bendera kwa mkono wa kushoto nao pia ukakatwa, Akashika bendera kwa vigutu na akaibana kwa kifua chake…! Mara ya tatu akampiga kwa mkuki bendera ikaanguka ikapaa roho ya Mus’ab kwenda katika Jannah ya milele, akiwa Shaheed…!

Baada ya kuisha vita, Mtume (saw) na Maswahaba zake walikwenda wakawaangalia Mashuhadaa walipofika katika mwili wa Mus’ab (ra) machozi mengi yaliwatoka…! Walipotaka kumkafini hawakupata ila kijishuka kilikuwa wakikieka kichwani miguu inakua wazi, Na wanapo kiweka miguuni kichwa kinakuwa wazi…! Akasema Rasul (saw): “Kiwekeni upande wa kichwa na miguu muifunike na majani…!”

Kisha (saw) akaliangalia shuka lake alilokafiniwa akasema: “Hakika nimekuona Makkah na ilikuwa hakuna mwenye mavazi mazuri kukuliko, na manukato mazuri kukuliko. Kisha wewe ndiye huyu mwenye nywele tim tim katika shuka”. 

Itaendelea katika UQAB Toleo 14…In Shaa Allah.