Shambulizi La Riverside Lisitumike Kuendeleza Vita Dhidi ya Uislamu

Taarifa Kwa Vyombo vya Habari

Hizb ut Tahrir /Kenya imeshtushwa na mauaji ya watu 14 yaliyotokea katika hoteli ya Dusitd2 iliyoko eneo la Riverside, Nairobi. Sisi Hizb ut Tahrir /Kenya tunapinga vikali umwagaji damu na wakati huo huo tunasema yafuatayo:

Kwa kuwa kuna ripoti kuwa wahusika katika shambulizi hili wameuawa, tunatoa mwito kwa vyombo vya usalama nchini Kenya visiwasumbue raia wasiokuwa na hatia. Lakusikitisha imekuwa jambo la kawaida kwa polisi kuiandama jamii ya Waislamu kwa kisingizio kuwa wanaimarisha usalama.

Shambulizi hili la hoteli limetokea licha ya serikali kudai kuwa imeboresha usalama; hivyo basi, suali msingi ni: “Waliwezaje washambulizi hao kutumia gari lililokuwa na nambari za usajili za Kenya, kuingia hotelini na kufanya uovu huo? Tunasema kwa kinywa kipana kuwa ni jukumu la vyombo vya usalama kuhakikisha usalama kwa raia na mali zao.

Ama kuhusu vyombo vya habari vya humu nchini na vya kimataifa, vilipatiliza na kusema kuwa tukio hili ni kitendo cha ugaidi na kuwalaumu Waislamu na Uislamu kabla hata serikali kutoa kauli yake. Tunakichukulia kitendo chao hicho ni cha kimakusudi na kinalenga kuupaka matope Uislamu na kusababisha chuki za kidini kati ya jamii. Tunasema kwamba tawala za Kimagharibi hupatiliza mashambulizi mfano huu katika kuendeleza upotoshaji juu ya Uislamu kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Lakuvunja moyo zaidi, ni kwamba Wamagharibi katika kiu chao cha kupora mali za mataifa mengine, wanashirikiana na madikteta kufanya mauaji ya halaiki mfano Syria, Iraq, Sudan Kusini na maeneo mengine. Bila kuona haya, ugaidi wao wanauita ukombozi wa kumakinisha Demokrasia!

Kwa kutamatisha, tunatoa nasaha ya haki kwa Wasomi Waislamu wasiingie katika mtego wa Wamagharibi katika kuukashifu Uislamu kuwa ni chanzo cha ugaidi. Tunawakumbusha kuwa Wamagharibi hawatochoka katika kupambana na Uislamu na Vita dhidi ya Ugaidi vimelengwa kuwalazimisha Waislamu kuachana na mafunzo yao ya Kiislamu. Zaidi ya hayo, tunaamini kuwa wafuasi wa dini zilizopo hawatokubali mafundisho yao kuingiliwa au kubadlisha misimamo yao ya kidini kutokamana na kulazimishwa na wengine. Wamagharibi hawapigani na ugaidi wa kweli, bali wanawataka Waislamu wasijifunge kikamilifu na Uislamu wao kama mfumo bora na wenye uwezo wa kutatua matatizo yanayowakumba wanadamu leo. Hizb ut Tahrir /Kenya inasisitiza kwamba Uislamu tokea mwanzo hadi mwisho wa dunia, unapinga vitendo vyote vya vurugu ima vimefanywa na Waislamu au wasiokuwa Waislamu.

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari wa Hizb ut Tahrir Kenya

KUMB: 1440 / 04

Alhamisi, 11 Jumada I 1440H /

17/01/2019 M

Simu: +254 707458907

Pepe: mediarep@hizb.or.ke