Ubinafsi; Athari ya Mfumo Muovu wa Kirasilimali

Hakika hakuna tabia inayochukiza kwa mwanadamu na haswa Muislamu kama hii ya ubinafsi na uchoyo. Tabia hii imekithiri sana kwa mujtama wetu dhihirisho wazi la kufaulu kukubwa kwa mfumo wa kirasilimali; kukuuza na kueneza fikra zake potovu.

Leo urasilimali umetufikisha kiwango cha mtu kutomjali mpaka mzazi wake wala ndugu zake. Utaona pengine mzazi amehangaika kwenda mbio kumsomesha mtoto wake lakini pindi anapo fungukiwa maishani, hamjali tena mzazi yule bali hujali tu mke na watoto wake. Yuko radhi wazazi wake wafe njaa lakini hayuko radhi katu kugawanya pato lake ili kuwakimu wazazi wake licha ya kuwa wao pia ni mas’uliya yake kuwaangalia na atahisabiwa juu ya hili.

Ama kwa ndugu na jamaa wa karibu, neema aliyofunguliwa na Allah (swt) ya mali hayuko tayari pia kuwasambazia na kuwanufaisha licha ya kuwaona wazi kuwemo katika hali ya dhiki na ufukara. Je, ni nini kinachomfanya huyu kutowasaidia nduguze? Si jengine ila ni fikra potovu ya kirasilimali ya ubinafsi nayo ni kuwa: akili yake na maarifa yake ndiyo yaliyo mneemesha na kwamba kila mtu ale bidii ya jasho lake, na yeyote asiye changia katika uzalishaji hana nafasi ya kuendelea kuishi. Amekosa kutambua kuwa riziki ni miongoni mwa mambo yaliyomo ndani ya mzunguko unaomtawala mwanadamu na kwamba hana khiari wala kauli juu yake. Bidii, akili wala maarifa sizo zenye kudhamini riziki ya mtu bali ni maagizo tu tuliyo agizwa kuyatekeleza. Lau kama haya ndiyo yanayo dhamini riziki, ni wangapi wenye akili, maarifa na bidii ambao hawana riziki? Na kinyume chake ni wangapi wamefunguliwa riziki na Allah pasi na kuonekana werevu wala wenye maarifa? Hivyo basi mtoaji ni Allah (swt) pekee humpa anaye mtaka apendavyo Yeye pasi na hisabu. Hakika ya Mali ni mtihani; leo unayo kesho huna. Hivyo basi yatakikana uwapendelee wenzako mazuri kama unavyo jipendelea mwenyewe.

Kutokana na hali ya ugumu wa kimaisha leo chini ya ubepari wa kirasilimali, kila mmoja anahisi kubanwa. Hali hii imepelekea mpaka kukosa wa kukunyoshea mkono pindi unapo hitaji msaada wa dharura. Kwa kuwa serikali za kirasilimali hazidhamini ushibishaji wa mahitajio ya watu binafsi, kamwe hazijishughulishi kuinua hali ya raia mafukara chini yake bali jukumu hili hubwagiwa mashirika yasiyo ya kiserikali. Hili husababisha hata wenye nacho nao kuingiwa na hofu lau watatoa kusaidia, keshoye nao watasaidiwa na nani? Hali hii pia tunaishuhudia mpaka ndani ya majumba kati ya ndugu na jamaa wa familia moja.

Tamati

Kwanza, tutambue kuwa mali ni amana kutoka kwa Allah (swt) na ni miongoni mwa mitihani ya Allah kwa waja wake; ima ikunufaishe au ikuangamize hapa duniani na kesho akhera. Uislamu huhimiza utoaji katika kheri kwa watu jumla lakini haswa kwa ndugu na jamaa wa karibu kwa kuwa katika hili kuna ujira mara mbili: malipo ya sadaka na malipo ya kuunga kizazi. Wekeza mali yako zaidi katika akhera yako kwani Mtume (saw) asema katika hadithi ya Abu Huraira (ra) kuwa mali yako ni moja kati ya mambo matatu; yasiyo kuwa hayo ni mali ya warathi wako:

‹‹يَقُولُ الْعَبْدُ مَالِي مَالِي إِنَّمَا لَهُ مِنْ مَالِهِ ثَلاَثٌ مَا أَكَلَ فَأَفْنَى أَوْ لَبِسَ فَأَبْلَى أَوْ أَعْطَى فَاقْتَنَى وَمَا سِوَى ذَلِكَ فَهُوَ ذَاهِبٌ وَتَارِكُهُ لِلنَّاسِ››

“Mja anasema: mali yangu mali yangu, hakika mali yake ni katika mambo matatu tu; alicho kula kikamalizika au alicho vaa kikachakaa au alichotoa akakiweka (kesho akhera) yasiyo kuwa haya ataondoka na kuwaachia watu (warathi)” [Muslim].

Pili, fikra ya ubinafsi na uchoyo kwa kuhofia kufilisika katika kutoa katika kheri haina msingi katika Uislamu. Bali Allah ametuahidi ukitoa katika kheri atakulipa maradufu na zaidi na pia atatufanyia wepesi mambo yetu. Allah (swt) asema:

فَأَمَّا مَنْ أَعْطَىٰ وَاتَّقَىٰ  *وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَىٰ * فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْيُسْرَىٰ

Basi kwa mwenye kutoa na akawa na uchaji Mungu* Na akalisadikisha jema* Tutamsahilishia wepesi.

[Al-Layl: 5-7]

Tatu, hali hii haiwezi kubadilika kikamilifu kwa watu kwa kuwa mfumo tawala leo wa kirasilmali ndio unao wasukuma watu – kupitia kumakinisha fikra hii potofu ya ubinafsi mabongoni mwao – kuwa na tabia hizi za kinyama, wala hakuna njia mbadala ya kusafisha haya isipokuwa kwa kuung’oa mfumo huu batili na kurudisha Uislamu kama mfumo badala na wenye haki yake chini ya serikali ya Khilafah, utakao wachochea watu – kupitia mtazamo wake sahihi kuhusu riziki na mali – kuwa wakarimu katika utoaji mali zao kwa lengo la kupata radhi za Allah (swt). Hali hii itajenga mapenzi na uwiano mwema kwa mwenye nacho na asiye kuwa nacho na kudhamini maisha ya raha na utulivu. Hili hatimaye litasababisha kuwepo fungamano imara baina ya raia ndani ya serikali ya Khilafah na kuwawezesha kusimama pamoja dhidi ya adui wao, hivyo basi kuregesha tena izza kwa Uislamu na Waislamu.

Kufikia kwenye izza hii hatuna budi ila kujizatiti na kutia juhudi na uwezo wetu kulingania mabadiliko ya kimfumo na kufanya kazi kwa ikhlasi na harakati ya Kiislamu ya kiulimwengu ya Hizb ut Tahrir kuregesha Khilafah Rasheeda ‘Ala Minhaj an-Nubuwa ya pili kama alivyo tuahidi Rasullah (saw).

Mohammad Bates (Abu Imad)