Ufupisho wa Hotuba Ovu ya Macron dhidi ya Uislamu na Waislamu

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron mnamo Ijumaa, 2 Oktoba 2020 katika Kasri la Elysee alitoa hotuba ya kihistoria na yenye chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu. Hotuba hiyo ilipeperushwa ulimwenguni kote.  Hotuba hiyo ilikuwa inafuatia ziara ya Macron nchini Lebanon mnamo Jumanne, 1 Septemba 2020; ambapo alizungumza kuhusu kwa nini hakulikashifu jarida la vichekesho la Charlie Hebdo kwa kuchapisha tena vibonzo vya kukufuru dhidi ya Mtume wetu Muhammad (saw). Alisema, “Sio nafasi ya rais wa Jamhuri kutoa hukumu juu ya maamuzi ya mwandishi wa habari au idhaa ya habari, la. Kwa sababu tuna uhuru wa vyombo vya habari.” (Reuters, 15/09/2020).

Hotuba hiyo iliangazia tishio la unaoitwa Uislamu wa kujitenga. Ilisisitiza mwito kwa taifa kujikusanya na kuchangamkia uamsho unaolenga kulinda maadili na misingi ya jamhuri ya kisekula ya Kifaransa ambayo yanashambuliwa na Uislamu mkali.  Kwa kuongezea aliliomba taifa kumuunga mkono yeye na Serikali yake katika mchakato wa kuja na mswada mkali ambao utapelekwa katika Baraza la Mawaziri mnamo Ijumatano, 9 Disemba 2020 na Waziri na Naibu Waziri wa Ndani ili upitishwe kabla kupelekwa Bungeni kwa mjadala na kupitishwa kuwa sheria.  Mswada huo unatajwa kuwa ni uboreshaji wa sheria ya mwaka 1905 na inalenga kuuboresha usekula na kuyajumuisha maadili ya jamhuri.

Sheria hiyo itakuwa ndio marudio ya kimkakati yatakayojumuisha nguzo tano muhimu zifuatazo:

Kwanza, kuweka hatua ambazo zitapigia debe kutoegemea mrengo fulani katika nyanja ya utulivu wa umma na huduma za umma. Hatua hizo zinalenga kutatua sintofahamu zinazoshuhudiwa aghalabu na wale wanaotaka na wanaotoa huduma za umma kama vile huduma za kuogelea na mabasi. Kwa mfano, baadhi ya Waislamu wanadaiwa kutaka wapewe huduma kwa upendeleo kwa kudai wanawake na wanaume watenganishwe na watengewe muda tofauti katika sehemu za kuogelea.  Kwa upande mwingine, wengine wanafanyiwa ubaguzi kutokana na mavazi yao na hivyo kunyimwa nafasi katika huduma za usafiri.  Hivyo basi, hatua hizo zitalenga kuzisawazisha jinsia zote pasina kuzingatia dini zao kwa kuwa Ufaransa ni jamhuri ya kisekula.

Pili, kuboresha udhibiti wa miungano ndani ya ardhi ya Ufaransa na kuhakikisha kuwa ipo kwa ajili ya kuhudumikia na kupigia debe misingi ya jamhuri ya kisekula ya Kifaransa. Kwa kuongezea, ili kuziwezesha asasi za Dola katika kutia saini na miungano na kuipa misaada ya kifedha kwa sharti kwamba haikiuki maadili ya jamhuri ya kisekula ya Kifaransa.  Lau itakwenda kinyume na makubaliano ya mkataba, basi irudishe pesa na itakabiliwa na kuvunjwa.

Tatu, ili kuziboresha sheria za mwaka 1882 na 1969. Kiudhati ni shule ndani ya Jamhuri ndio chungu cha kuyeyusha. Zaidi ya hayo, shule ndiyo inayoasisi usekula na kuhifadhi maadili ya jamhuri ndani ya mioyo na akili za wanafunzi. Watoto wanalindwa dhidi ya ushawishi wa dini kupitia kwenda shule. Hivyo basi, kuanzia mwanzo wa kalenda ya masomo ya 2021, kila mmoja kuanzia miaka 3 lazima aende shule na kusoma nyumbani hakutoruhusiwa isipokuwa kwa udhibiti mkali tena kwa sababu za kiafya. Nidhamu ya elimu itakuwa moja pekee na ni ile ya EILE na ambayo itakuwa chini ya udhibiti mkali wa Waziri wa Elimu ya Kitaifa nchini Ufaransa. Masomo ya kufundishwa lazima yakuze mapenzi kwa jamhuri ya kisekula na kupigia debe hisia za uhuru. Shule zote lazima zijifunge na maelekezo ya maadili ya jamhuri ya kisekula ya Kifaransa na lau zitakiuka zitafungwa.

Nne, kujenga Uislamu unaooana na maadili na misingi ya kijamhuri ya kisekula ya Kifaransa. Ili kuwa na Uislamu wa Kifaransa, Waziri wa Ndani atafanyakazi na Baraza la Ibada la Waislamu nchini Ufaransa ili kupambana na ushawishi kutoka ng’ambo. Jamhuri ya Ufaransa imeamua kusitisha kwa amani kuwafunza na kuwaleta maimamu kutoka Uturuki, Moroko na Algeria ndani ya ardhi ya Ufaransa. Kutakuwepo na udhibiti na utekelezaji mkali wa sheria ya mwaka 1905 kuhusiana na udhamini wa kifedha kutoka ng’ambo kwa misikiti. Baraza la Ibada la Waislamu nchini Ufaransa litaweka mpango wa kuwafunza na kuwapigia debe maimamu na wasomi ambao watautetea Uislamu unaooana na maadili ya kisekula ya Kifaransa. Baraza la Ibada la Waislamu nchini Ufaransa litaorodhesha kozi za mafunzo, litatoa vyeti kwa maimamu, litaandaa mkataba ambao maimamu wakiukiuka watafutiliwa mbali na watapangilia namna ya utekelezaji wa safari ya hajj kwa ajili udhamini wa dharura wa kifedha kutoka kwa jamhuri ya Kifaransa. Hatimaye, Jamhuri itatoa msaada kwa miradi iliyoanzishwa na Waqf wa Uislamu nchini Ufaransa wa kitita cha uro milioni 10 katika nyanja za thaqafa, historia na sayansi.

Tano, ili kuangazia uwezo na ushindi wa Jamhuri dhidi ya Uislamu pale ilipoiangamiza Dola ya Kiislamu ya Khilafah mnamo 3 Machi 1924 na kusimamisha juu ya ardhi yake ambayo ilikuwa imeungana lakini Jamhuri na washirika wake wakaigawanya kuwa vijidola 54 na kuweka juu yake nidhamu ya kijamhuri iliyopo mpaka leo. Hivyo basi, ahadi ya Jamhuri lazima ihuishwe kwa kuzitekeleza sheria zake kwa ukali na hatimaye mapenzi na mustakbali wa Jamhuri utashinda.

Kwa kutamatisha, ufupisho huo hapo juu unafichua wazi kufeli kamili kwa mfumo wa kirasilimali wa kisekula na nidhamu zake zenye sumu katika kutoa usalama na ustawi wa kweli kwa wanadamu. Majanga yao na kufeli kwao kunashuhudiwa duniani kote na kuzidishwa na janga linaloendelea la Covi-19 ambalo limesambaratisha hadhara ya Kimagharibi ambayo inanawiri kwa msingi wa ubaguzi wa rangi na pengo la tajiri na masikini.  Kwa upande mwingine, Uislamu unachomoza duniani kote na muda wowote kuanzia sasa utakuwa ndio nguvu kuu ya kisiasa katika ulingo wa dunia.  Kwa hiyo hizo patashika mpya kutoka kwa jamhuri ya Kifaransa, mlinzi wa makubaliano ya Sykes-Picot ambayo ndio chanzo cha mauaji na uporaji usioingia akili wa rasilimali za Mashariki ya Kati hadi Afrika.  Uongozi wa Kifaransa unajulikana daima kwa namna unavyo kwenda mbio kujipa sura mpya kila unapokabiliwa na majanga ili kuwahadaa watu kuwa upo imara lakini kiuhalisia unatapatapa kubakia usije ukatumbukia. Hatimaye, Macron anadanganya alipotangaza kwamba Uislamu upo katika janga, ilhali uhalisia unaonyesha kinyume.  Ukweli ni kwamba mfumo wa kirasilimali wa kisekula upo katika chumba cha mahututi unasubiri kutangazwa kifo chake kwa kuwasili kwa Khilafah iliyosimama kwa njia ya Utume.  Kwa kuwa Uislamu ndio njia pekee mbadala yenye uwezo na iliyowahi kujaribiwa kutatua matatizo ya wanadamu wote pasina kuzingatia rangi, dini au vyeo vyao. Kwa hiyo uongozi wa Kifaransa umejitwika kampeni na njama ovu ambazo daima zimefeli kwa misingi ya kirongo kwamba Uislamu ni mkali na Waislamu ni watu wenye misimamo mikali ili kuweza kuwakatisha watu tamaa ili wasiukumbatie! Sasa ndio wakati wa #KurudishaKhilafah. قَدۡ بَدَتِ ٱلۡبَغۡضَآءُ مِنۡ أَفۡوَٲهِهِمۡ وَمَا تُخۡفِى صُدُورُهُمۡ أَكۡبَرُ‌ۚ “Imekwisha fichuka chuki yao katika midomo yao. Na yanayo ficha vifua vyao ni makubwa zaidi.” (Aal-e-Imran: 3: 118).

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir