UHURU

Haambwi mwanadamu, kwa Molawe yuko huru, kufanya anavyotaka,

Ni mja ajifahamu, isimpate ghururu, kwambaye ni makhaluka,

Alowekewa nidhamu, nyoofu kama sururu, kutoka kwake Khalika,

Kufata nafsi sumu, kiholela bila nuru, nuru inayomulika,

 

Kiumbe hujidhulumu, mwenyewe akajidhuru, amuaswipo Malika,

Na awe mustakimu, Mungu aloyaamuru, ajipinde kuyashika,

Yeye duniani humu, kapawa ikhtiyaru, si uhuru kwa hakika

Uhai si wa kudumu, alanao ashukuru, ni ghafula hukatika,

 

Neema zake Karimu, kwa wajawe ni kathiru, si zenyi kuhisabika,

Shukura yawalazimu, wala wasizikufuru, zisijezikatoweka,

Akili ilotimamu, kawatunuku jabbaru, mambo yapatetujika,

Halali ama haramu, haipangi ni kufuru, silo la kukubalika,

 

Kateuzwa binadamu, kati ya kheri na sharru, ipi atayoinyaka,

Mwenyewe hutakadamu, matendoni akaduru, atendalo likatuka,

Huongozwa na fahamu, alonazo na fikiru,  hazawi nazo khuluka,

Kukumbushana dawamu, ni wajibu na ni birru, kwenye dini bila shaka,

 

Huyu mwana wa Adamu, katukuzwa na Swaburu, umbo zuri kaumbika,

Muongozo ulotimu, peke utamnusuru, asipatekuhilika,

Ela akiuhujumu, tini kuliko himaru, kidaraja atashuka,

Aweje ja bahaimu, amayu samaki nguru, thamani walodunika?

 

MTUNZI – MOHAMMED BAKARI 

 

ALMUFTI 

 

MOMBASA – KISAUNI