Vurugu ni Jambo la Kawaida Katika Mfumo wa Kisekula wa Kirasilimali

Wakenya wanafuatilia kwa makini matukio ndani ya sekta ya elimu kuhusiana na utekelezwaji wa mtaala mpya. Lakini walio makini zaidi ni wazazi, walimu na wachapishaji ambao wameshtushwa na mkanganyiko wa kauli zinazotoka kwa washikadau wa elimu wakiongozwa na Wizara ya Elimu. Mnamo Jumanne, 11 Disemba 2018, Waziri wa Elimu aliiambia Kamati ya Elimu ya Seneti kuwa serikali inasitisha utekelezwaji wa mtaala mpya kutokana na kukosekana kwa mashauriano ya kina, maandalizi na mafunzo kwa walimu. Kisha siku ya Jumamosi, 15 Disemba 2018, Waziri wa Elimu akiwa pamoja na Katibu wake na washikadau wengine katika elimu baada ya kuwa na mkutano wa faragha ndani ya Taasisi ya Maendeleo ya Mtaala ya Kenya alitoa kauli kuwa mtaala mpya utazinduliwa rasmi kwa ukamilifu mwaka 2020 na sio 2019 kama ilivyopangiliwa hapo awali. Maamuzi yalitokana na ripoti ya wakaguzi huru ambao walipata udhaifu kadhaa katika mtaala huo ikijumuisha kukosekana kwa fehda, miundo mbinu duni ya shule na mafunzo yasiyokuwa na mpangilio kwa walimu. (Daily Nation, 17/12/2018)

Malalamiko yakafuatia kutoka kwa wazazi na wachapishaji ambao walihisi kuwa wamefanyiwa khiyana kwa kuwa walikuwa washanunua vitabu na wametumia pesa nyingi katika kuchapisha ala za kusomea mtawalia. Waziri wa Elimu akatoa kauli tena Jumamosi, 22 Disemba 2018 na kusema kwamba Januari 2019 wizara itaanzisha rasmi kwa umakini mpangilio wa mtaala mpya kuanzia chekechea (pre-primary I and II) hadi darasa la 1, 2 na 3. Lau kama mtaala huo utaanza rasmi unaweza kukumbwa na matatizo kwa kuwa hakuna Sheria ya Sera ya Kitaifa ya Mtaala na Nakala ya Mabadiliko ya Mtaala wa Elimu na Mafunzo, ambazo kufikia sasa hazijafikishwa mbele ya Bunge ili kupitishwa. Hii ikimaanisha kuwa litakuwa zoezi kinyume na sheria mpaka Bunge liidhinishe vipengee hivyo viwili kabla tarehe 3 Januari 2019 ambapo shule zitakuwa zinafunguliwa. (Daily Nation, 22/12/2018). Zaidi ya hayo, Muungano wa Wakitaifa wa Walimu (KNUT) ulisema kuwa hawakushauriwa kutokana na maamuzi ya hivi majuzi na hivyo wanapinga uzinduzi huo wa mtaala mpya Januari 2019 mpaka serikali itatue mapungufu yaliyoelezewa na wakaguzi. Mambo yalizidi unga Jumanne, 24 Disemba 2018 pale Baraza la Magavana (Cog) liliposema kuwa hawana pesa za kufadhili mtaala huo mpya. (Daily Nation, 24/12/2018)

Ni wazi kwamba tawala za kisekula za kirasilimali zinaendeshwa kwa kutegemea fujo kwani mfumo wenyewe wa kisekula wa kirasilimali unatokamana na fujo. Hivyo basi, kila kitu chake ikijumuisha sera zinazotokamana nao ni maslahi na vurugu kwa sababu ya itikadi yake ya kisekula ambayo imelitoa jukumu la Muumba la kuwatungia wanadamu sheria na badala yake wanadamu wanajitungia sheria wenyewe. Ni jambo lakusikitisha kuona kwamba sera muhimu na ambayo inaathari kubwa katika nyanja zote za maisha inashuhudia mkanganyiko aina hii. Kutoelewana huko kunatokana na kuwa washikadau wengi katika elimu wanajali tu maslahi yao ya kibinafsi hususan wachapishaji kwa ushirikiano na serikali ambao watatia mabilioni ya fedha kutokana na kuchapisha ala za masomo. Zaidi ya hayo, watawafunza watoto wetu wachanga fikra ovu za kisekula za kirasilimali ambazo wamezitoa kutoka kwa mabwana zao wamagharibi wakoloni na ambazo zitawajenga na kuwafanya kuwa watu masekula wenye akliyya (akili) na nafsiyya (utendaji) zinazosukumwa na madaniyya (mali/vitu vya kushikika)! Malengo yao maishani ni kujistarehesha kwa upeo wa juu! Kipimo chao cha vitendo ni maslahi! Hivyo basi, wanaandaliwa kuja kuendeleza vurugu la usekula ndani ya jamii yao!

Suluhisho msingi liko katika kuukumbatia ulinganizi wa kurudisha tena maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha Khilafah kwa njia ya Utume. Ni kupitia Khilafah pekee ndiko kutakakopelekea wanadamu kufikia amani, utulivu na ustawi wa kweli. Kwani Khilafah itatekeleza sera zote ikijumuisha ile ya elimu kwa mujibu wa Qur’an na Sunnah na sio kwa mujibu ya wanavyotaka wamagharibi wakoloni na mfumo wao batili wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake chafu. Nidhamu ya elimu katika Khilafah itajikita katika kujenga Utambulisho wa Kiislamu (Shaksiyyatul Islam). Utambulisho wa kipekee ambao unahakikisha kuwa wanafunzi wanakuwa na akliyya na nafsiyya ya Kiislamu, ambao malengo yao maishani ni kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Zaidi ya hilo, kipimo chao cha vitendo ni Halali na Haramu. Kwa maana nyingine, wanaandaliwa kuwa watumwa wa Mwenyezi Mungu na hatima yake ni jamii iliyotulivu hapa duniani na pepo akhera.

Ali Nassoro Ali

Mwanacha wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya