Deni ni Njia ya Halali ya Kumiliki Mali

Ufupisho wa Suali na Jawabu – 7

Suali:

Kwa mujibu wa Kitabu cha Nidhamu ya Uchumi Katika Uislamu cha Hizb ut Tharir kimenukuu kuwa njia za kumiliki mali ni tano: Kazi, Urathi, Haja ya mali kwa ajili ya uhai, Ruzuku ya mali kutoka kwa serikali kwa raia na mali anayoyapata mtu bila kutoa mali au juhudi.

Je mfano mtu anapokopesha Ksh1000 kutoka kwa mtu mwengine. Kisha akanunua mzigo sokoni na akauuza na kupata faida ya Ksh.500. Kisha akamregeshea aliyemkopesha Ksh.1000 zake na yeye akabakia na Ksh.500 alizopata kama faida. Kwa hiyo yaliyotokea ni njia ya kumiliki mali? Au ilikuwa njia ya kuzidisha mali?

Jibu:

Pesa anazopewa mtu kama mkopo ni mali yake punde tu anapozitia mkononi, na anaruhusiwa kuzitumia atakavyo bila kizuizi, mfano anaweza kuzitoa kama zawadi, au kuzitumia yeye na familia yake au kuzifanyia biashara. Hayo hayaathiri makubaliano ya yeye kuzirudisha kama malipo ya mkopo wake kwa aliyemkopesha.

Lau mtu huyo atatumia pesa alizokopa katika kufanya biashara, atakuwa anafanya kitendo cha kuzidisha rasilimali, na biashara yake itakuwa ni njia ya kuzidisha mali na sio njia ya kumiliki mali. Maanake asili ya pesa hizo ni za yule mfanyi biashara ambaye ndiye aliyekopeshwa, hivyo basi faida atakayopata katika biashara ni uzidishaji wa pesa zake asili na wala halitojumuishwa katika njia za umilikaji. Hili linadhihirika wazi lau mwenye deni atapata hasara katika biashara, na hasara hii itahusiana na hasara juu ya pesa zake na sio pesa za aliyemkopesha. Kwa sababu aliyemkopesha bado anadai deni lake kamili kwa mujibu wa makubaliano licha ya kupata faida au hasara katika biashara yake.

Hivyo basi kukopesha pesa ni njia ya kumiliki mali nayo inaingia katika kitengo cha tano ambacho ni “Mali anayomiliki mtu bila kutoa mali au juhudi”. Kwa sababu inamruhusu anayekopeshwa kumiliki pesa na kuzitumia kwa mujibu wa hukm za Kiislamu.

Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye Hekima.

Link ya Kiengereza: http://hizb-ut-tahrir.info/en/index.php/qestions/ideological-questions/8018.html

Chanzo: Hizb ut Tahrir Kenya

21 Shaaban 1439 Hijria

07 Mei 2018 Miladi