“Na nani aliye mbora zaidi katika Kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu”

Wakenya tokea tarehe 9 Machi 2018 wamekuwa wakishuhudia mijadala kuhusu mchakato wa kura ya maoni juu ya kubadilishwa kwa katiba. Ndani ya mijadala hii kuna kambi mbili; kwanza matajiri ambao wanatofautiana katika maslahi ima kufanyike au kusifanyike kura hiyo. Pili ni ile ya walalahoi ambao wameandaliwa kikabila na kieneo kujisalimisha kwa matajiri ili wawatumikie kama ngazi ya kufikia malengo yao. Baadhi ya madai ya umuhimu wa kura hii ni:

Kwanza, kubuni vyeo ambavyo vitahakikisha kuwa hakuna mizozo baada ya kila uchaguzi; kwa kuwa walioshindana kila mmoja atapata nafasi fulani katika mamlaka. Ukweli ni kwamba hata kukabuniwa vyeo kiasi gani kattu havitokidhi kiu ya mamlaka ya washindani walafi masekula.

Pili, kupunguza gharama ya juu ya uwakilishi na usimamizi katika serikali za Kaunti, serikali ya Kitaifa, Bunge la Kitaifa na Seneti n.k. Ukweli ni kwamba katiba mpya ya 2010 ndiyo iliyobuni muundo huu mpya na nafasi zake.

Tatu, kuupa nafasi uchumi kukua kwa kuwekeza katika mipango ya maendeleo jumla. Ukweli ni kwamba asilimia kubwa ya mapato (ushuru na mikopo) imekuwa ikiibwa na kinachobakia kinafanyiwa ubadhirifu wa hali ya juu n.k.

Madai hayo ni ya uongo maanake kiasili yamechipuka kutokana na kipimo cha maslahi. Kipimo hicho kinatokana na mfumo unaotutawala wa urasilimali uliochipuza kutokana na itikadi ya kisekula (kutenganisha dini na maisha/serikali). Mfumo tuliourithi kutoka kwa wakoloni wamagharibi umempa mwanadamu jukumu la kujitungia sheria (katiba) kwa mujibu wa akili yake finyu kinyume na maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu. Hivyo basi, walioko mamlakani daima hupatiliza fursa kutunga au kufanya mabadiliko ili kukidhi maslahi yao!

Mfano maarufu ni kipindi cha miaka 15 ya utawala wa Jomo Kenyatta, Katiba ya Lancaster kutoka Uingereza ilifanyiwa mabadiliko mara 16! Baadhi ya mabadiliko yalikuwa ni kumfanya Jomo Kenyatta kuwa Rais kutoka kuwa Waziri Mkuu, kuivunja Seneti, kuwafunga pasi na kuwapeleka mahakamani wale wote wanaoushtumu utawala wake n.k. Na kipindi cha utawala wa Moi alibadilisha Katiba na kuifanya Kenya kuwa nchi ya chama kimoja na KANU chama tawala pekee! Kwa upande mwingine Katiba ya 2010 ilipigiwa debe na Marekani na kuchukua muundo wa Marekani kwa kuwa Raila kibaraka wao alitarajiwa kuchukua uongozi lakini mara akazidiwa maarifa na Uingereza na hivyo UhuRuto wakachukua mamlaka kwa kutumia propaganda za uwiano na muungano wa makabila hasimu nchini kutoka Central na Rift Valley!

Kama yalivyokuwa Mabadiliko ya Katiba ya hapo awali si tu nchini Kenya bali hata Marekani; pamoja na haya mapya kattu hayatarajiwi kuwa ni kwa ajili ya kuwajali raia katika kuwalainishia kitanzi cha mzigo wa maisha kooni! Bali utabakia kuwa ni mpango wa walafi wachache kutumia kura hii ya maoni kufikia maslahi yao kwa kuwatumia walalahoi katika kuyahalalisha maslahi yao kwa kushiriki zoezi hilo! Je wakati haujafika wa sisi kuachana na hukumu za mwanadamu na kuchukua za Mwenyezi Mungu? Kwa kujiunga na ulinganizi wa kurudisha tena maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha Dola ya Kiislamu ya Khilafah kwa njia ya Utume. Khilafah itakayo hukumu kwa Qur’an na Sunnah. Kipimo chake kikiwa ni Halali na Haramu; na lengo la maisha ni kumridhisha Mwenyezi Mungu. Khilafah ndio mbadala pekee yenye uhakika.

وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللهِ حُكْماً”
“Na nani aliye mbora zaidi katika kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu”

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya