Nidhamu ya Kijambazi Inayo Wapora Raia Wake

Habari:

Watumizi wa umeme wanakabiliwa na deni la bili za nyuma la shilingi 8.1 bilioni huku kampuni ya Kenya Power ikichukua hatua za kumudu gharama za matumizi ya mafuta ya dizeli katika mitambo ya uzalishaji umeme za mwaka jana na ambazo haziku jumuishwa katika malipo ya kila mwezi huku serikali ikigharamia mahitaji ya umma katika mwaka wa uchaguzi. Kenya Power ilidhihirisha kuwepo na mzigo mkubwa wa gharama zake katika taarifa yake ya fedha ya kila mwaka, ikieleza kuwa hii ilitokamana na ukame mkali mwaka jana, iliyopelekea udharura wa ongezeko la uzalishaji ghali wa umeme kwa njia ya dizeli uliofidia upungufu mkubwa wa uzalishaji umeme kwa njia ya maji. Gharama hii ni sehemu ya shilingi 10.1 bilioni zilizo tambuliwa kama gharama za mafuta katika uzalishaji umeme ambazo bado kampuni ya serikali ya Kenya Power haijazirudisha katika taarifa yake ya fedha ya kila mwaka ya mwezi Juni 2017. Takriban shilingi 2 bilioni zimerudishwa kufikia sasa, huku shilingi 8.1 bilioni zikisukumiwa wateja katika bili zao za kila mwezi.

Maoni:

Punde tu baada ya tangazo la Kenya Power kuhusu mipango ya kurudisha kiasi hicho cha gharama, takriban jumla ya Wakenya walijibu kwa njia ya kutoridhika katika mitandao ya kijamii kupitia anwani #switchoffKPLC dhidi ya mipango hiyo na kila mmoja wao alikashifu wazo kuhusu jinsi gharama hiyo kubwa ilivyo patikana! Serikali ya Kenya kupitia Waziri wa Kawi Charles Keter baada ya kutambua kuwa ripoti iliyotolewa na Kenya Power; haikupokewa vyema na umma ilijiingiza kwa upole kuokoa sura ya serikali ambayo huenda ikakabiliwa na mashtaka mahakamani juu ya hilo. Bwana Keter alisema kwamba kubadilika badilika kwa malipo katika gharama za umeme kuliko hisiwa na wateja hivi majuzi kulitokana na kuwepo kwa mfumo wa utoaji bili usiokuwa madhubuti unaofanya usomaji wa mitambo ya mita kwa njia ya ukisiaji tu badala ya kuchukua vipimo halisi!

Kutia msumari kidonda, serikali ilifichua kwamba bili za umeme kwa wananchi wenye pato la chini huenda zikaongezeka kuanzia Aprili 2018 huku malipo kwa wenye mapato wastani yakitarajiwa kushuka kwa kutarajiwa kumalizika kwa ruzuku kwa wateja wadogo! Kwa sasa serikali imewagawanya raia katika vigawanyo vifuatavyo:

  1. Watumizi wa chini hutumia nyuzi 50 kwenda chini kwa mwezi na wanalipishwa shilingi 2.50 kwa nyuzi (kWh) moja kwa saa.
  2. Watumizi wastani hutumia baina ya nyuzi 51 – 1,500 kwa mwezi na wanalipishwa shilingi 12.75 kwa nyuzi
  3. Watumizi wa juu hutumia 1,500 na kwenda juu kwa mwezi na wanalipishwa shilingi 20.57 kwa nyuzi

Taarifa hizo za juu zinathibitisha kuwa katika nchi yoyote ya kirasilimali utoaji huduma ni njia ya biashara na wala sio jukumu jumla kwa serikali yoyote juu ya raia wake. Iweje kampuni ya serikali mithili ya Kenya Power itangaze faida ya shilingi 7.27 bilioni huku raia ambao walitakiwa wawe wamiliki wa kampuni hii wanateseka juu ya malipo makubwa kwa msingi wa vigawanyo hivi ambavyo hakukuwa na usemi wao katika kuundwa kwake? Jibu ni makampuni katika serikali za kirasilimali yanajulikana kumilikiwa na serikali katika waraka pekee lakini kiuhalisia, yanasimamiwa na kuendeshwa na warasilimali walafi kwa jina la wawekezaji. Wanaoitwa wawekezaji ndio wanao dhibiti taasisi za kiserikali na kutekeleza sera zinazo kusudia kuwapendelea wao na kuhakikisha kuwa wanapata migao ya juu ya faida kutokana na hisa wanazomiliki. Hii imepelekea raia kuteseka katika sekta zote mfano ikiwemo ya afya ambapo raia wasiokuwa na bima kama ile ya afya ya kitaifa almaarufu NHIF hawakubaliwi au kutibiwa katika mahospitali, sera za elimu huundwa kuwapendelea wawekezaji katika sekta hiyo kiasi ya kuwa elimu bora kamwe sio kigezo kinachotumiwa katika upimaji sera!

Suluhisho la kipekee ni kubadilisha nidhamu hii ya kijambazi ya kidemokrasia na mfumo wake batili wa kirasilimali inayotokamana kwayo. Nidhamu inayo nawiri kupitia kuwafanyia unyama raia wake na kutazama utoaji huduma kama chimbuko la pato na miradi kuundwa ili kufuja mali ya umma kwa ajili ya maslahi ya kibinafsi. Kulingania kubadilishwa kwa nidhamu aina hiyo sio tu ni kadhia ya dharura bali ni hitajio litakalo leta amani, utulivu na ufanisi kwa raia wote ambao kamwe hawata gawanywa kwa msingi wa mapato yao. Hilo laweza pekee kupatikana chini ya nidhamu adilifu ya utawala iliyojengwa kutokana na mfumo safi wa Kiislamu kwa Njia ya Mtume (saw). Khilafah (nidhamu ya utawala ya Kiislamu) daima itakuwa inajitahidi kumridhisha Allah (swt) na kuwa na hamu ya baraka zake na rehma zake ili kuingizwa katika pepo yake ya juu. Kwa kuzingatia hilo, watawala ndani ya Khilafah watashajiishwa kwa utoaji hudumu halisi na kilicho cha Umma kitatambuliwa kwa uhalisia kuwa cha Umma na kutumiwa na kupewa kipaumbele kukidhi mahitaji ya raia kwa msingi wa maoni yao.

Enyi Wakenya, mpaka lini mutateseka kutokana na usaliti huu wa kiuchumi kutoka kwa serikali yenu wenyewe? Huu ni unyama kuona kuwa maisha yenu daima yamejaa mateso; licha ya mishahara duni ambayo wachache wenu walio bahatika kuajiriwa wanapokea; bado wanapanga njama ya hata kukichukia hicho kidogo munacho kihifadhi kupitia ushuru wa kila aina ambao mumeangaziwa kwao? Tunawalingania kutafakari kwa makini juu ya hali muliyoko nayo kwa sasa na mustakbali wa watoto wenu na wajukuu zenu na kisha mujiulize nafsi zenu; je, hakuna suluhisho msingi la kudumu? Kwa moyo mkunjufu tunazielekeza nyoyo zenu na akili zenu zilizo na ikhlasi kuupa Uislamu fursa na kuusoma kama mfumo ulio teremshwa kwa Mtume Muhammad (saw) ili kuendesha mambo yote ya maisha ya wanadamu kwa mfumo huo.

Enyi Waislamu, mpaka lini mutashabikia nidhamu iliyo kinyume na yale yaliyo teremshiwa kipenzi chenu Rasulullah (saw)? Je mumetosheka pekee na vibahashishi ambavyo mfumo huu muovu na batili wa kirasilimali unawarushia mikononi mwenu na kutupilia mbali furaha ya milele katika mabustani ya Jannatul Firdaus? Sisi ndugu zenu tumefungua mikono yetu na kuwalingania katika kazi iliyo bora zaidi iliyo tawazwa kwa Mitume ya kuongoza Umma kutoka katika giza kwenda katika nuru. Giza la utawala wa kirasilimali na itikadi yake ya kiilamaniy iliyo sababisha leo majanga ya kila siku duniani. Ili kwa pamoja tulinganie badali ya giza hili kuwa nuru ya Uislamu kama mfumo utokao kwa Muumba wa mwanadamu. Nuru itakayo angaza majumba yote yakiwemo majumba ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu kutokana na rehma za Muumba kwa viumbe vyake.

Ali Nassoro

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

http://www.nation.co.ke/news/Why-Sh8-1bn-has-been-slapped-on-power-bills-/1056-4251366-6xw93hz/index.html

http://www.nation.co.ke/news/Electricity-bills-will-not-be-backdated-Energy-CS-Charles-Keter/1056-4255806-yok4mdz/index.html

http://www.nation.co.ke/news/Poor-homes-to-pay-more-for-electricity/1056-4256474-oos5asz/index.html

Kutoka Jarida la UQAB Toleo 13