Vurugu na Ghasia ni Sarafu Moja ya Pande Mbili za Siasa ya Demokrasia

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari:

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’I, ameshtumu vikali kitendo cha kushambulia msafara wa Naibu Rais William Ruto katika eneo la Magharibi mwa Kenya kilichofanyika tarehe 23 Oktoba, 2021. Magari kadhaa ya naibu raisi kwenye msafara huo yaliharibiwa na kundi la vijana walioonekana wakipinga ziara yake ya Mji wa Busia. Tayari washukiwa wanane wa ghasia wametiwa mbaroni. Wazushaji rabsha hizi walikuwa ni vijana waliokuwa wakipiga kelele za miito ya chama cha ODM huku wakirushia mawe msafara wa Naibu Rais. Matiang’I alionya kuwa serikali haitomvumilia yeyote yule atakayevuruga mikutano ya kisiasa.

Maoni:

Kenya haijasalimika kutoka kwa kampeni chafu zinazonuka uvundo za chaguzi za Kidemokrasia. Huku uchaguzi mkuu ukikaribia, wanasiasa wamo kwenye mchakamchaka wakijipigia debe na vyama vyao au miungano yao ya kisiasa semi za chuki pamoja na ghasia kutoka kwa wanasiasa hawa wa kidemokrasia ni zenye kurindima. Naibu Rais licha ya kuandamana na wabunge wa maeneo bunge ya magharibi wakiwemo John Waluke, Fred Kapondi, Majimbo Kalasinga, Dan Wanyama, Didmus Barasa, Mwambu Mabonga, Benjamin Washiali na aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale, hilo lote halikuzingatiwa wala kusitisha wafuasi wa mrengo mwengine wa kisiasa katika kuutupia mawe msafara wake.

Machafuko na fujo ni kama sarafu moja yenye sura tofauti za Demokrasia. Palipo na Demokrasia utakuta pia vurugu, vita na kila aina ya uasi sheria ni wenye kutawala. Hii inaweza kushuhudiwa tangu kuibuka kwa mfumo wa kidemokrasia duniani mwaka 1789, kufuatia Mapinduzi ya Ufaransa. Ulimwengu ulishuhudia vitendo vya ukatili ambavyo havijawahi kushuhudiwa ikiwa ni pamoja na kumwaga damu za watu wasio na hatia hasa za mapadri na makasisi.

Walioitwa wanamapinduzi walikuwa na mwito wa kinyama wa kuwataka rai wawanyonge wafalme na malikia kwa matumbo ya kasisi wa mwisho watakayempata!! Haya yalifanywa huku Siasa ya Kidemokrasia ikaibuka kama suluhu mbadala na kusheheni fujo kama sifa yake ya kudumu. Kwa mfano aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump aliposhindwa kwenye uchaguzi wa 2020 aliwachochea wafuasi wake kusababisha ghasia na fujo. Wafuasi wake hao walisababisha vurugu na fujo na wakajaribu pia kuvamia majengo ya Seneti.

Huu ni mwanzo tu. Mabaya zaidi yanatazamiwa wakati wa uchaguzi utakapofanyika na matokeo kutangazwa. Joto, shauku na taharuki hupanda zaidi na kuibua wasiwasi wa kutokea fujo na ghasia.

Vitendo hivi vya kishenzi kwa hakika ni janga ambalo sio tu limekithiri katika nchi za kidemokrasia wakati uchaguzi unapokaribia. Dalili ya wazi ya jinsi kampeni za kidemokrasia zinavyosababisha vurugu na vita hata kabla ya matokeo ya uchaguzi ambapo baadhi ya wagombea wanakataa kukubali kushindwa. Ikiwa bado uchaguzi haujafanyika lakini tayari twaona visa vya vurugu na uvunjaji wa sheria vinashuhudiwa.

Kampeni za kidemokrasia zimeshindwa kabisa kuwaunda watu kwenye mshikamano na kuwaunganisha kwa pamoja kwa amani chini ya mwavuli mmoja wa amani kama taifa imara moja.

Imeandikiwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Hussein Muhammad Hassan

Mwanachama wa Afisi ya Habari Hizb ut Tahrir Kenya