Bajeti ya Kenya ya Mwaka 2018/2019: Adhabu ya Kila Mwaka Kutoka kwa Serikali ya Kisekula ya Kikoloni kwa Watumwa Wake

Habari na Maoni

Habari:

Hazina ya taifa imesema inatarajia kodi ya (PAYE) kukua kwa shilingi bilioni 68 na kufikia shilingi bilioni 447.6 katika mwaka ujao wa matumizi ya serikali, ikiashiria kujitolea kwake kushinikiza ahadi ya muda mrefu ya marekebisho kwa sheria ya ushuru wa mapato. [Chanzo: Business Daily Africa)

Maoni:

Wakenya daima huwa na matarajio kila taarifa za sera ya bajeti (BPS) zinapotolewa kabla ya kuwasilishwa bajeti halisi bungeni. Hii imetokana na kule kuwa maisha yao tayari ni mabaya sawia na ule msemo kuwa wao ni msumari baina ya mbao na nyundo! Hali ya Kenya ni mbaya mno kiasi ya kuwa kwa sasa inateseka kutokana na mafuriko, baa la njaa, kudorora kwa sekta ya afya, kuporomoka kwa sekta ya elimu, viwango vya kushtua vya ukosefu wa ajira, kashfa za uporaji wa rasilimali za umma, serikali iliyo zongwa na mrundiko wa madeni yanayo kisiwa kufikia shilingi trilioni Ksh.5 nk.

Kenya kama serikali yoyote ile ya kisekula ulimwenguni kuwepo kwake kunategemea vyanzo viwili vya mapato ambayo ni ushuru na mikopo ya riba inayo chukuliwa kutoka kwa taasisi za kifedha za ndani na nje ya nchi. Raia hulipa ushuru kwa njia ya moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia mikopo ya riba. Machimbuko mawili haya hutia uzani mkubwa juu ya mabega ya raia wasiokuwa na njia badala za kujikimu badala yake kutegemea ‘wawekezaji’ warasilimali masekula wa kikoloni ambao haja yao ni kazi za kitumwa zenye mishahara duni na faida kuu! Kiasi ya kuwa hali ni mithili ya chawa baina ya vidole viwili, ambapo kazi hizo za kitumwa hulipwa mishahara duni kwa malengo mawili lile la kuhakikisha wanapata tonge tu ili waishi na kuendelea kuwafanyia kazi wawekezaji, na kulipa ushuru ili kuendesha serikali ya kisekula!

Kenya imebarikiwa na rasilimali nyingi ikiwemo ardhi yenye rutuba, madini, mafuta nk iliyo na uwezo wa kugeuza uchumi wake na kutupilia mbali mizigo ya ushuru na mikopo ya riba. Lakini, shina la hali yake mbaya hii ni kuukumbatia kwake mfumo wa kisekula wa kikoloni wa kirasilimali ambao juu yake imebuniwa nidhamu ya kiuchumi. Nidhamu ya kiuchumi ya kirasilimali inajali tu ukuaji wa uzalishaji jumla wa nchi (GDP) kiasi ya kuwa kuna tabiri na tafiti za kiuchumi zinazouonesha uzalishaji jumla wa Kenya kukua kwa tarakimu 2. Serikali ili kuhakikisha inafikia ukuaji huu wa tarakimu 2 inawashawishi wawekezaji kwa kuwapa muamala wa nafuu na kutafuta kuidhinishwa na Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) kama taifa lenye thamani kifedha na kiuwekezaji. Huku ikifeli kumaliza umasikini, ukosefu wa ajira, baa la njaa nk kupitia utozaji wake wa ushuru na njia ya mikopo ya riba. Kuhalalilsha kufeli kwao kwa kutaja kauli mbiu ya uchumi wa kirasilimali kuwa tatizo la kiuchumi la jamii ni uhaba wa bidhaa na huduma ikilinganishwa na mahitaji. Hii yamaanisha kuwa tatizo hili halitibiki na litaendelea kuwepo daima.  Ukweli ni kuwa ni majambazi wa kirasilimali wachache wanaomiliki na kuficha mabilioni ya rasilimali kwa gharama ya wengi wanaoshirikiana kwa kichache baina yao! Kwa hivyo katika serikali za kisekula kila mmoja na nafsi yake na hakuna kutarajiwa nusra kwa serikali inayo kupora moja kwa moja kupitia utozaji ushuru na kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia kulipa madeni yake!

Uislamu chini ya Khilafah (Dola ya Kiislamu) itakayo simamishwa tena kwa njia ya Mtume (saw), utatekelezwa kwa ukamilifu ikiwemo nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu inayo tokamana nayo. Sera ya kiuchumi ya Kiislamu itakuwa ni kudhamini ushibishaji wa mahitaji yote msingi kwa kila mtu kikamilifu, na kumwezesha kushibisha mahitaji yake ya ziada kwa kadri anavyoweza kama mwanadamu anayeishi katika jamii fulani iliyo na nidhamu maalumu maishani. Hiyo yamaanisha Khilafah itayashughulikia matatizo msingi ya kila mtu kama mwanadamu, anayeishi kwa mujibu wa mahusiano fulani, kisha kuwawezesha kuinua kiwango cha maisha yao na kufikia utulivu wao wenyewe kwa mujibu wa muundo fulani maishani. Hivyo basi, nidhamu ya kiuchumi ya Kiislamu ni ya kipekee na ni tofauti na sera nyenginezo za kiuchumi zilioko leo duniani.

Katika Khilafah (Dola ya Kiislamu) itakayo simamishwa tena kwa njia ya Mtume (saw), kila mtu mwenye uwezo atawajibishwa kufanya kazi kukidhi mahitaji yake msingi na ya wanaomtegemea. Kwa upande mwengine, watoto au warathi watawajibishwa kuwasaidia wazazi wao ikiwa hawawezi kufanya kazi, au Hazina ya Dola (Bait ul-Mal) inawajibishwa kuwasaidia wazazi ikiwa hakuna wa kuwasaidia. Kwa msingi huo, Uislamu wamuhitaji mtu kudhamini kushibisha mahitaji yake msingi na ya wanaomtegemea yaani chakula cha kutosha, mavazi na makao, na una muwezesha mtu kudhamini mahitaji ya ziada maishani kwa kadri anavyoweza.

Katika Khilafah (Dola ya Kiislamu) itakayo simamishwa kwa njia ya Mtume (saw), ushuru na mikopo ya riba ni haramu. Utozaji ushuru ni katika hali zisizo za kawaida ambazo ni wajibu juu ya Waislamu wote kuzisimamia kwa mfano ukame au Jihad. Ushuru huchukuliwa tu juu ya mali iliyo zidi matumizi ya kawaida ya mtu katika kushibisha mahitaji yake msingi na ya ziada. Hivyo basi, inatimiza haki ya riziki kwa kila mtu kibinafsi, na kurahisisha kudhamini mahitaji ya ziada. Wakati huo huo Uislamu umeweka mipaka fulani ambayo kwayo mtu anaweza kuchuma ili kushibisha mahitaji yake msingi na ya ziada na kupanga mahusiano yake na wengine kwa mujibu wa nidhamu maalumu.

Mwamko wa Kenya na Afrika jumla uko katika kubadilisha mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake chafu zitokanazo nao ikiwemo ile ya kijambazi ya demokrasia, nidhamu nyanyasaji ya kiuchumi na uhuru wa kijamii nk, ambazo ndizo chanzo cha mateso yake na majanga yanayo ziathiri. Badala yake, kukumbatia mradi wa Khilafah chini ya ulinganizi wa mwamko wa Kiislamu, ambao kwa sasa umezagaa kote duniani na ambao kusimamishwa kwake tena kwa njia ya Mtume (saw) kutaipeleka Kenya na Afrika katika hadhara kuu iliyo sheheni utulivu, amani na ufanisi ambayo kamwe hayajawahi kushuhudiwa katika zama zote za utawala wa kisekula wa kikoloni!

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

#SimamisheniKhilafah