BATUK – Zana ya Kikoloni yenye Kulinda Maslahi na Ajenda ya Kikoloni

Habari:

Mnamo Jumanne, 6 Aprili 2021, Mkuu wa Majeshi ya Uingereza Jenerali Bwana Nick Carter alizuru Kenya na kumtembelea Mkuu wa Majeshi Jenerali Robert Kibochi katika Makao Makuu ya Jeshi huko Nairobi. Wawili hao walijumuika katika maongezi ya pamoja kuhusiana na ushirikiano baina ya majeshi ya mataifa hayo mawili.

Jumanne mchana, Jenerali Bwana Nick alitoa hotuba kuhusu Mchakato wa Usalama wa Kimataifa katika Chuo cha Ulinzi wa Kitaifa akiwa mwenyeji wake ni Kamanda, Luteni Jenerali Adan Mulata. Hatimaye, mnamo Jumatano, alikamilisha ziara yake kwa kuzuru Kitengo cha Mafunzo cha Jeshi la Uingereza (BATUK) huko Nanyuki ambako alijuzwa kuhusu mafunzo na mazoezi ya kijeshi ya pamoja ambayo wanajeshi wa Uingereza hushiriki wanapokuwa Kenya. (https://mod.go.ke)

Maoni:

Bila shaka ziara hii ilikuwa ni ya hatua iliyozingatiwa kwa kina na bwana mkoloni Muingereza ili kuwatuliza mameneja wake vibaraka watiifu. Hii ni baada ya matukio matatu nyeti yanayochipuza kutoka Uingereza. Kwanza – ni tukio la wanajeshi wa Uingereza kuleta nchini Kenya aina ya virusi vya Covid-19 kutoka Uingereza vinavyojulikana kama B.1.1.7 walipokuwa wanakuja kwa mafunzo. Pili – moto mkubwa ulioanza mnamo Jumatano, 24 Machi 2021. Wanajeshi wa Uingereza chini ya BATUK walisababisha moto mkubwa walipokuwa mafunzoni kwa kinachodaiwa kuwa ni kifaa cha ulipuzi kilichoboreshwa. Moto huo ambao ulichukua takribani siku 5 kuuzima, uliharibu zaidi ya ekari 12,000 za Mlima wa Loldaiga.

Hayo yalipelekea shirika la kimazingira, Kituo cha Kiafrika kwa ajili ya Hatua za Kurekebisha na Kuzuia (ACCPA) kulishtaki Jeshi la Uingereza kwa tukio hilo. Kwa kuongezea, ACCPA ilitoa ombi kwa BATUK na Hifadhi ya Loldaiga kuwapa fidia wenyeji walioathirika na madhara ya kimazingira yaliyo sababishwa na moto huo. Tatu – ilani isiyoingia akilini dhidi ya usafiri kwa Kenya iliyotolewa na Uingereza na kuisababisha serikali ya Kenya kulipiza kisasi!

Kenya ni taifa huru katika karatasi lakini ni koloni la Uingereza katika muktadha halisia. Kando na kuwa Kenya ni mwanachama wa Jumuiya ya Madola, imeidhinisha makubaliano yanayoitia minyororo Kenya kwa bwana wake mkoloni. Baadhi ya mikataba hiyo ni Makubaliano ya Ushirikiano wa Kijeshi na Uingereza ambao upo zaidi miaka 40! Katika mpango huo wanajeshi wa Uingereza wanatakiwa kuwepo nchini Kenya kwa ‘sababu za kimafunzo.’

Kwa hiyo, imepelekea zaidi ya wanajeshi 10,000 wa Uingereza kufanya mafunzo nchini Kenya kila mwaka! Kwa maandalizi ya kutumwa katika maeneo yenye anga sawia nayo kama Afghanistan na Iraq. Hivyo basi, BATUK ni kitengo cha kudumu chenye kutoa msaada kilichoko haswa Nanyuki kikiwa na kambi ndogo huko Kahawa. Kwa kuongezea, Uingereza inayo Timu ya Uingereza Yenye Kutoa Msaada kwa Afrika Mashariki (BPST-EA). Lengo lake ni kuratibu msaada wa kijeshi wa Uingereza kwa vikosi vya kijeshi ndani ya Afrika Mashariki kama vile Mafunzo kwa AMISOM Kabla-Kutumwa vitani n.k.

Inafahamika kuwa yeyote anayedhibiti jeshi ndiye anayedhibiti taifa. Kwa kuwa Uingereza inapatiliza mahusiano yake ya kikoloni kwa Kenya na ambayo ushawishi wake unapenya ndani ya safu za muundo wa Jeshi ambao msingi na mawe ya ujenzi wake yamewekwa na yeye.  Mwishowe malengo yake ni kulinda maslahi na ajenda yake nchini Kenya na ndani ya eneo pana la Afrika Mashariki. Hivyo basi, vita dhidi ya ‘Ugaidi’ na ‘Misimamo Mikali’ vinatoa fursa ya dharura muhimu ili kuendeleza kasi za mipango ya kijeshi hususan sasa hivi ambapo Uingereza imetoka ndani ya Muungano wa Ulaya (EU).

Uingereza iko mbioni kujiweka vizuri ili kupangilia sera na mbinu zake ili kuweza kunyanyua haiba yake inayodorora ikiwa pweke hivi leo. Kwa hiyo, haya makosa mapya yaliyojitokeza kutoka upande wa Uingereza ni upepo dhaifu vilivyostahiki ziara ya siku mbili kutoka kwa Mkuu wa Majeshi ya Uingereza ili kuwatuliza mameneja katika shamba la kikoloni. Hali itabakia kama ilivyokuwepo awali kama inavyothibitishwa na ukimya wa Wizara za Majeshi na Mazingira kuhusiana na kelele kutokana na uharibifu uliofanyika kwa mazingira. Pia, mzozo wa kidiplomasia utafifia.

Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Ali Nassoro Ali

                                       Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir