Tusiwe kama Mwanamke asokotae uzi wake bar’abara kisha akaanza kuufumua tena!

Siku ya kwanza ya Shawwal huwa Waislamu husherehekea sikuu ya Idul-Fitr ishara ya kumalizika kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Hekima ya Idd kutanguliwa na swala kwanza kabla ya khutba ni kutakiwa Waislamu kufanya haraka kushukuru fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yao ya kuwezeshwa kukamilisha ibada ya Swaum kupitia kitendo cha Swala. MwenyeziMungu aliwataka Waislamu watukuze jina Lake baada ya kukamilisha kwao ibada tukufu ya swaumu.

ولِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ
Na mtimize hesabu yenu na kumtukuza MwenyeziMungu kwa kuwa amekuongozeni ili mpate kushukuru.
[Al-Baqarah: 185]

 Waislamu wamekua wakijipata kwenye mzozo juu ya suala la  kusherehekea Idi kufuatana na suala la muandamo wa mwezi. Ikhtilafu ya Mwezi ambao kiasili ni suala la Kifiqhi lenye rai mbili juu yake.

Rai ya kwanza; Waislamu hulazimika kufunga au kufungua kwa mujarad wa kuandama mwezi mahala popote duniani.

Rai ya pili; ni kufunga na kufungua kuambatana na muandamo wa mwezi wa eneo lao (Matlai). Tofauti hii haianzi leo ila tofauti ilioko sasa na ile ya zamani ni kua suala la mwezi leo limechovywa siasa ndani yake. Baada ya Waislamu leo kujipata wakiishi katika nchi zenye mipaka ya kitaifa ya Sykes –Pikot (Mpango wa kikoloni wa kugawanya dunia ile Wakoloni waweze kuendeleza utawala wao duniani). Suala hili limefanya kila nchi iweze kuwa mamlaka maalumu ya kutangazia Waislamu wa nchi hiyo siku ya Kufunga na siku ya kufungua. Linalopaswa kueleweka hapa ni kuwa, Kiislamu suala la Ikhtilafu lolote lile hukabiliwa kwa njia mbili msingi nazo:-

Kwanza: Kuheshimiana kirai na hii endapo kila mmoja atabeba rai tofauti na mwenzake. Hata hivyo ni muhimu pia kufahamu kwenye rai mbili kuna moja huwa lazima ni nzito  zaidi kuliko nyengine yaani uwezekano wa kuwa moja wapo ina makosa.

Pili; suala lolote ambalo Waislamu hutofautiana likiwa linapekelea kuhujumu umoja wa umma wa Kiislamu, kuna ufaradhi wa kuweko na mwenye kukata kauli moja naye ni kiongozi (Khalifah) aliyepewa mamlaka ya kutabanni (Kuteua rai moja miongoni mwa rai ambazo watu hutofautiana kisha akalazimisha Waislamu wote wabebe rai hiyo). Kinyume na Khalifa hakuna Muislamu yoyote anayeruhusiwa kulazimisha watu rai yake. Kwa kuwa misingi hii leo imepuuzwa na haifanyiwi kazi basi tutaendelea kushuhudia mikwaruzano na mabezano miongoni mwa Waislamu mambo ambayo yenyewe hayafai Kiislamu.Idd sio sherehe tu bali ni moja wapo ya ishara muhimu za umoja wa Kiislamu ambao kwa bahati mbaya maadui wanaufanyia kila njama kuuhujumu.

Shawaal ni mwezi wa kumi katika kalenda ya Kiislamu yenye mezi kumi na mbili. Siku ya kwanza ya mwezi huu huwa ni Idul Fitr inayojumuisha Waislamu wote katika furaha baada ya kukamilisha faradhi ya swaum. Allah ameufanya mwezi huu uwe baina ya Mwezi wa Ramadhan na ule wa Dhul Qa’da. Ikumbukwe kuwa Dhul Qa’ada ni miongoni mwa miezi minne mitukufu ndani yake haifai kudhulumu nafsi zetu. Nao pia ni mwezi wa maandalizi wa Ibada ya Hajj. Kwa maana hii baada ya Waislamu kutoka katika mwezi  Ramadhani wenye fadhila chungu nzima, huingia katika mwezi wa Shawwal ambao siku yake ya kwanza tu ni miongoni mwa siku bora duniani. Na baada ya mwezi huu, Waislamu huingia kwenye miezi mitatu mitukufu yenye kufuatana; Dhulqa’da, DhulHijja na Muharram.Kupewa misimu yote hii ni kutakiwa kuipatiliza nafasi ya kufanya mema pasina na kuchoka. Hakika MwenyeziMungu ametutaka tuishi na Uislamu hadi mwisho wa pumzi zetu.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ))

Enyi Mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha wala msife isipokuwa mmekwishakuwa Waislamu kamili. [Al-Imran:102]

 Ramadhani ni mgeni huja na kutoka nasi pia ni wageni hapa duniani tumekuja na tutaondoka hivyo tunatakikana kujipinda kwa kujikusanya yatakayotufaidi hapa duniani na kesho Akhera. Ole wao wale wenye kughurika na maisha ya dunia wakasahau kuwa wamo safarini. Hakika sio katika wema watu kujichaguliwa msimu wa kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Hakika sio katika wema kujiweka huru wa kumuasi Mungu kwa hoja kuwa Ramadhani imekwisha. Kinachotakikana ni kuendelea na kufanya mema tuliyokuwa tukiyafanya ndani ya Mwezi wa Ramadhani swala za usiku, kudumu kuswali swala za jamaa na kufunga sunna ikiwemo zile siku sita za Shawal. Hakika alama moja ya kukubaliwa Ramadhani zetu ni kuendelea zaidi na mema tuliokuwa tukiyafanya Ramadhani kinyume chake ni ishara mbaya ya kuwa Ramadhani zetu zimekuwa na mushkila endapo tumerudia mabaya tuliyoyaacha ndani yake. Waislamu hawafai kusitisha maovu bali wanatakikana kuyaacha kabisa kama vile vile hawatakikani kufanya baadhi ya mema na kuacha baadhi yake.

أَفَتُؤْمِنُونَ بِبَعْضِ الْكِتَابِ وَتَكْفُرُونَ بِبَعْضٍ ۚ فَمَا جَزَاءُ مَن يَفْعَلُ ذَٰلِكَ مِنكُمْ إِلَّا خِزْيٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يُرَدُّونَ إِلَىٰ أَشَدِّ الْعَذَابِ ۗ

Je Mnaamini baadhi ya Kitabu na kukataa baadhi yake basi hakuna malipo kwa mwenye kufanya haya katika nyinyi ila fedheha katika maisha ya dunia na siku ya Qiyamah watapelekwa katika adhabu kali. [Al-Baqara:85]

Tuwe na tahadhari na Sheitani ambaye kwa sasa amefunguliwa na atakua na kasi kubwa mno ya kututelezesha misimamo yetu.Tusirudie maasia tuliyoyahama ndani ya Mwezi wa Ramadhani kwani kufanya hivyo ni sawa na yule mwanamke aliekua akiiusokota uzi wake bar’abara na kuwa mgumu kisha aanza kufungua tena kwa kuukatakata vipande!

Shabani Mwalimu

Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari

Hizb ut-Tahrir Kenya.