Uhuru wa Kuzungumza ni Hadaa ya Serikali za Kisekula za Kirasilimali

Habari:

Mnamo Jumatano, 16 Mei 2018, Raisi wa Kenya alitia saini kuwa sheria Mswada wa Matumizi Mabaya ya Tarakilishi na Uhalifu wa Mitandao, 2018. Zaidi ya hayo, mnamo Jumanne, 22 Mei 2018, Bodi ya Kuratibu Filamu ya Kenya (KFCB) ilitoa ilani kuwa kuanzia tarehe 28 Mei 2018, yeyote atakaye rekodi video kwa ajili ya watazamaji jumla atahitajika kupata leseni kwa hilo.

Maoni:

Serikali zote za kisekula za kirasilimali ikiwemo Kenya hunawiri kwa ‘kuupa umaarufu uhuru’ utokanao na akili finyo ya mwanadamu kwa jina la sheria iliyojengwa juu ya stakabadhi za kikatiba. Sheria za kisekula zina sifa ya kufanyiwa marekebisho ili kubeba maoni tofauti tofauti lakini yenye kutegemea uongozi ulioko mamlakani. Uhuru wa kuzungumza hukubaliwa tu wakati unaafikiana na serikali ilhali chochote kilicho kinyume na serikali hakikubaliwi. Ama kuhusu sheria hizi mpya zilizotiwa saini zina malengo mawili msingi:

Kwanza, kuzuia upinzani wowote dhidi ya dosari za serikali km. kuwahisabu watawala wanapofeli katika mujukumu yao, kufichua ufisadi katika taasisi za umma pamoja na taasisi za kibinafsi nk.

Pili, kuweka kikwazo dhidi ya mazungumzo yoyote ya kuleta mfumo badili dhidi ya mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake zilizovunda km demokrasia, uhuru wa kijamii, nidhamu dhalimu za kiuchumi ambazo zote zimeshindwa vibaya kusimamia mambo ya wanadamu. (Cyberterrorism – Ugaidi wa mitandaoni). Kama ilivyothibitishwa na Kiongozi wa Wengi Bungeni aliyesema: “Mswada huu utawashughulikia wale wote wanaotumia teknolojia kuwapa misimamo mikali vijana wetu ili kuingia katika ugaidi”

Malengo hayo mawili msingi yame nukuliwa kwa mukhtasari katika sehemu zifuatazo:

Sehemu ya 22(1): Mtu yeyote atakaye dhamiria kuchapisha takwimu za kirongo, za kupotosha au za uzushi au za kimakosa kwa nia kwamba takwimu hizo zichukuliwe au kufanyiwa kazi kama zilizo sahihi, kwa mapato ya kifedha au pasi na mapato ya kifedha, anafanya kosa na atakapopatikana na hatia, atawajibika kulipa faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo cha muda usiozidi miaka miwili, au yote mawili.

Sehemu ya 23: Mtu anayechapisha habari kwa kujua kuwa ni ya urongo, kwa maandishi, utangazaji, takwimu au kupitia mfumo wa tarakilishi, itakayopelekea hali ya taharuki, vurugu au ghasia miongoni mwa raia wa Jamhuri, au inayoweza kuharibu hadhi ya mtu anafanya kosa na atakapopatikana na hatia, atawajibika kulipa faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo cha muda usiozidi miaka kumi, au yote mawili.

Hilo ndilo umbile la sheria chini ya serikali za kisekula za kirasilimali, hupitishwa, kurekebishwa na kufutiliwa mbali kwa msingi wa maslahi, matakwa na matamanio ya hali halisi ambayo hutumikia maslahi ya serikali za kikoloni za kisekula za kirasilimali za kimagharibi zinazoongozwa na Amerika, Uingereza na washirika wake.

Sheria hizi zilipitishwa licha ya kukashifiwa vikali na katika enzi ambazo hakuna ‘chama imara cha upinzani’ kudhibiti mamlaka ya serikali ya kupita kiasi’. Hii ni baada ya kuthibitishwa uhalali wa serikali ya Kenya (Jubilee) kupitia kule kupeana mikono kati ya Raila Odinga (kiongozi wa upinzani) na Uhuru Kenyatta na ambako kulifunga hatima ya mamilioni ya wafuasi wa siasa za upinzani. Sheria hizi zilizopitishwa zilifuatiwa na simu kutoka kwa Waziri wa Amerika Mike Pompeo kwa Raisi Kenyatta mnamo Ijumaa, 18 Mei 2018 ambapo walijadiliana kuhusu “malengo ya ushirikiano wa kupambana na ugaidi, kuimarisha usalama wa eneo na kuhakikisha utawala mzuri”.

Kenya ikiwa kama kitovu cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) cha Afrika na kupenya kwa kwa sekta ya hali ya juu ya intaneti na simu-hodari; wakati huo huo ikiwa mbele katika kupigana vita vya Kimagharibi kimwili nje ya mipaka yake kwa jina la kupigana na ugaidi na kindani ikipigana vita vya kifikra kwa jina la misimamo mikali na uvukaji mipaka. Ili kuhalalisha kujitolea kwake na juhudi zake kwa mabwana wake wa kikoloni wa Kimagharibi, ilipitisha mswada huu kuwa sheria ili ipeane jukwaa la kutafuta misaada ya wafadhili wa Kimagharibi na usaidizi jumla wa kutekeleza sheria hii mpaka mwisho wake.

Utulivu, amani na ufanisi ambazo Kenya na Afrika yote unahitaji mno uko katika kubadilisha kwake mfumo wa kisekula wa kirasilimali na nidhamu zake zilizovunda, ambazo ndio sababu ya mateso yao na kulemaa kwao kisiasa, kijamii na kiuchumi kulikosababishwa na wakoloni wa Kimagharibi. Ukombozi wao wa kimfumo uko katika kuukumbatia mradi wa Khilafah unaolingania Mwamko wa Kiislamu utakaopelekea kusimama tena kwa Khilafah katika njia ya Mtume (saw). Chini ya Khilafah wakoloni wa Kimagharibi na mfumo wao wa kisekula wa kirasilimali barani Afrika watafurushwa na uwezo halisi wa Afrika kupatikana kwani maadui halisi wa Afrika watakuwa washafukuzwa nje ya mipaka yake na hivyo basi ufanisi utakuwa ni jambo la kutarajiwa.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Ali Nassoro Ali

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

  1. https://www.standardmedia.co.ke/article/2001280622/uhuru-signs-into-law-computer-and-cybercrimes-bill
  2. https://www.techweez.com/2018/05/22/kfcb-licensing-regulations-kenyans-react/
  3. https://www.npr.org/sections/thetwo-way/2018/05/19/612649393/kenyas-crackdown-on-fake-news-raises-questions-about-press-freedom
  4. https://www.nation.co.ke/news/Trump-s-top-diplomat-assures-Uhuru-of-US-support/1056-4569478-177oy6z/index.html