Vyombo vya Dola Tanzania Vyawatia Nguvuni kwa Uonevu na Dhulma Wanachama Watatu wa Hizb Ut-Tahrir

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Hizb ut-Tahrir Tanzania inalaani vikali kitendo cha dhulma na uonevu kilichotendwa na vyombo vya dola kuwatia nguvuni wanachama wake watatu, kuwashikilia kisiri bila ya maelezo au mashauri ya wakili zaidi ya mwezi kinyume cha sheria kisha kuwabambikizia kesi za hatari na uwongo ati ‘kula njama kwa ajili ya ugaidi’ na ‘kutekeleza kitendo cha kigaidi’. Mashtaka haya maovu kabisa ya uzushi na yasiyokuwa na kichwa wala miguu!

Wanachama waliotiwa nguvuni ni Waziri Suleiman Mkaliaganda (31) mwalimu wa sekondari aliyenyakuliwa tangu tarehe 21/10/2017 nje ya msikiti wa karibu na nyumbani kwake, eneo la Mtwara mjini, kusini mwa Tanzania, kisha kufuatia na wengine wawili Omar Salum Bumbo (49), fundi mwashi aliyenyakuliwa na maafisa wa usalama tangu tarehe 27/10/2017 kisha akafuatia Ustadh Ramadhan Athuman/Ustadh Moshi (37), mwalimu wa dini na mfanyabiashara aliyenyakuliwa mnamo tarehe 30/10/2017 nyumbani kwake. Matukio ya wawili (Umar Salum na Ustadh Moshi) yalitendeka jijini Dar es Salaam.

Omar Salum Bumbo alinyakuliwa na maafisa wa usalama, baada ya mmoja wa maafisa hao kwa ujanja kumuahidi Omar wakutane eneo fulani kana kwamba angetaka kumpatia kazi ya ujenzi. Baada ya Omar kufika eneo waliloahidiana kukutana, alitekwa nyara kwa mabavu na maafisa hao, kumsweka garini, kisha kutoweka nae, huku wakimtisha dereva wa boda boda aliyemfikisha eneo hilo kuondoka mara moja.

Amma Ustadh Ramadhan Moshi, licha ya kunyakuliwa nyumbani kwake mbele ya familia yake na kushuhudishwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Magomeni Makuti ‘A’ kisha maafisa wa usalama waliomkamata kuahidi kwamba taarifa zake zingepatikana katika kituo cha Polisi cha karibu. Kwa masikitiko makubwa wote wawili (Omar Salum na Ust. Ramadhan Moshi) zilipita wiki kadhaa bila ya taarifa za mahala walipo wala kujua mashtaka yao, licha ya jitihada kubwa ya familia na ndugu waliokuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya watu wao kufuatilia katika vituo mbalimbali vya Polisi. Kwa kipindi chote hiki walinyimwa haki zao msingi ikiwemo fursa ya uwakilishi wa kisheria (wakili).

Kufuatia qadhia hiyo, sisi Hizb ut-Tahrir Tanzania tunaanza kwa kuuliza, nani asiyejua dunia nzima kwamba tangu Hizb ut-Tahrir ilipoasisiwa imekuwa ikishikamana na njia safi na wazi ya ulinganizi wa mabadiliko ndani ya jamii kutoka kwa Mtume Muhammad SAAW, njia ambayo imefungika kwa kutumia upande wa kifikra na kisiasa tu bila ya kuhusisha utumiaji wa silaha, nguvu wala mabavu hata kwa siku moja? Njia isiyobadilika ambayo wanachama na wafuasi wote wa Hizb ut-Tahrir dunia nzima huwa ni sharti msingi kuiamini na kujifunga nayo na imefafanuliwa kwa kina katika vitabu na machapisho yake mbalimbali ambayo tunaomba jamii kusoma katika mitandao yetu ya kijamii iliyosambaa na maarufu ulimwengu kote.

Kisha tunauliza tena, jee vyombo vya usalama vilivyowatia nguvuni ndugu zetu, katika uchunguzi wao walipata fursa ya kupitia taarifa ya maelezo yetu yenye kufafanua malengo, njia na mwelekeo wa Hizb ut-Tahrir ndani ya Tanzania na ulimwengu mzima tuliyoyatoa kwa upana kupitia taarifa yetu kwa vyombo vya habari mara tu baada ya kongamano letu kubwa la wazi la kimataifa lililofanyika tarehe 19 Julai 2009 Msikiti wa Kichangani, jijini Dar es Salaam, na pia wanatambua kuwa sisi tumekuwa tukifanya kazi ya kulingania Uislamu kwa miaka mingi sana kwa uwazi katika jamii bila ya kujificha?

Tunaomba tena jamii kusoma taarifa yetu hiyo hapa :

http://www.hizb-ut-tahrir.info/…/press-rele…/kenyaa/392.html

Tena tunazidi kuuliza, jee vyombo vya usalama vinaelewa kwamba Hizb ut-Tahrir inafanya kazi ya kulingania Uislamu wazi kwa njia ya kifikra ulimwenguni kote zikiwemo nchi vinara wa kupambana na ‘ugaidi’ kama Marekani, Uingereza nk. Licha ya Hizb ut-Tahrir kufanya kazi ndani ya nchi hizo wazi wazi, hazijawahi nchi hizo hata siku moja kuinasibisha na kuihusisha Hizb ut-Tahrir na vitendo vya ugaidi ? Hivi Tanzania ina miundombinu imara na thabiti zaidi ya ulinzi, usalama, ujasusi na intelegensia kuliko nchi hizo kiasi cha kudiriki kuzua uwongo usiokuwa na kichwa wala miguu kwamba wanachama hao watatu wa Hizb ut-Tahrir wameshirikiana katika kitendo cha kigaidi?

Ikiwa huo unaoitwa uchunguzi haukuyazingatia hayo tuliyotangulia kuyataja, basi utakuwa uchunguzi wa aina gani kama si uonevu na dhulma zisizokuwa na msingi dhidi ya Uislamu, Waislamu na dhidi ya hao wanachama wetu watatu ambao ni maarufu kwa usafi wao ndani ya jamii kwa kujitenga kwao mbali na kila matendo ya vurugu, uhuni, uovu na ugaidi?

Hizb ut-Tahrir Tanzania tumeshasema mara nyingi na tunaendelea kupaza sauti yetu bila ya khofu wala kutafuna maneno kwamba Sheria ya Ugaidi ni sheria ya kibaguzi iliyolazimishwa na madola makubwa ikitumika kudhulumu,kueneza khofu, kutesa, kupoteza na kuulia jamii ya Waislamu ikiwemo pia kuwanyima haki yao msingi ya kutekeleza na kutangaza dini yao ipasavyo. Na kutiwa nguvuni wanachama wetu ambao hawana hata tembe ya kutenda wala kuamini matendo ya utumiaji nguvu na mabavu katika kulingania Uislamu, ni moja katika mifano mingi ya dhulma zinazowasibu Waislamu kutokana na sheria hii kandamizi.

Kwa kumalizia, Hizb ut-Tahrir Tanzania inatoa mwito (demand) kufutwa kwa mashtaka na kuachiwa huru mara moja wanachama wake bila ya masharti, kwa kuwa hawana makosa. Aidha, tunaomba viongozi wa jamii, wanafikira, waandishi wa habari na jamii kwa ujumla kushirikiana nasi kikamilifu katika kutangaza tukio hili na kushiriki katika kampeni ya kuachiwa huru ndugu zetu kutokana na dhulma na maonevu. Hapana shaka kila mtu makini anaelewa fika kwamba kuendelea kutumika kwa sheria hiyo kukandamizia Waislamu, sheria inayotukumbusha machungu ya zama za wakoloni mabeberu ni jambo linalotuburuza kuelekea mustakbali wa hatari, sio tu kwa Waislamu bali kwa ustawi wa uadilifu kwa jamii jumla

Afisi ya Habari

Hizb ut-Tahrir Tanzania

Kutoka Jarida la UQAB Toleo 12